Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri
Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika
Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za
Tanzania Bara kuwasilisha malalamiko yao ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi
kwenye Kamati za Maadili ngazi ya Kata na Jimbo zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza na Vyombo vya Habari leo
jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema kuwa NEC imepata taarifa kupitia Vyombo
mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo
vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya vitendo vyenye muelekeo wa
kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima amesema kuwa taarifa ya
Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017, imeeleza
kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma
waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya
afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kuwa Watendaji hao wana
lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya
Maadili ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na
malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani
viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata ndani ya saa
72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“ Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi
inaeleza wazi muda wa kuwasilisha malalamiko kwa kuvitaka vyama au wahusika
wenye malalamiko yoyote kuyawasilisha
kwa maandishi kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi husika ndani ya saa
72 tangu kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Tume inapenda kuvikumbusha vyama vya
Siasa kwamba, kwa mujibu wa sehemu ya 5.3 ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ambayo yalisainiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya Siasa, Chama cha Siasa au mgombea wa nafasi
husika anayeamini kwamba Maadili ya Uchaguzi yamekiukwa awasilishe malalamiko
yake katika Kamati ya Maadili ya ngazi
husika.
Hivyo, tunakishauri Chama cha ACT –
Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa
Jimbo la Dimani na vyenye Wagombea wa Udiwani katika Uchaguzi mdogo kwenye Kata
Ishirini (20) za Tanzania Bara kutumia haki yao kuwasilisha malalamiko ya
ukiukwaji wa Maadili katika Kamati husika.
Kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya
Maadili ya Uchaguzi, Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa, iwapo wana
malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani
kuwasilisha lalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya Kata saa 72 tangu
ukiukwaji huo wa maadili umefanyika.
Iwapo Chama cha Siasa au Mgombea
hataridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia
sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi awasilishe rufaa kwa Msimamzi wa
Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili
ngazi ya kata kutolewa.
Aidha, kama Chama cha Siasa
hakikuridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa
kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c) wanayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yao
katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa au ngazi ya Rufaa ambazo ni Tume ya
Taifa ya Uchaguzi.
Tunavishauri Vyama vya Siasa na
Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili ya Uchaguzi katika kuwasilisha
malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya
Maadili ya Uchaguzi, pale ambapo Chama cha Siasa au Mgombea hakuridhika na
maamuzi ya Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malamiko hayo ya
ukiukwaji wa maadili Mahakamani baada ya
Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya
Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.
Aidha, katika maelezo yao ACT
Wazalendo wameeleza tuhuma za wananchi kupokwa kadi zao za kupigia Kura. Nitoe
wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi ya
Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yako. Na
wananchi wasikubali kumpatia mtu yeyote kadi yao ya kupigia kura isipokuwa
kuionesha kwenye kituo cha kupigia kura siku ya kupiga kura tarehe 22 Januari,
2017.
Mwisho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi
kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya
Uchaguzi. Tume inaendelea kufuatilia kwa
karibu katika kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni. Haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote
atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment