Na. Aron Msigwa – NEC
10/1/2017. Dar es Salaam.
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wagombea na Vyama vya Siasa
vinavyoendelea na kampeni za Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Madiwani
kufanya kampeni za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Uchaguzi ya
mwaka 2015 na kwamba Chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo
atachukuliwa hatua.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji
Mkuu (Mst. Znz.) Hamid M. Hamid zikiwa zimebaki siku chache kabla ya
kufanyika kwa Uchaguzi huo Januari 22, 2017 kufuatia baadhi Vyama na
Wagombea kuanza kukiuka Maadili na taratibu za Kampeni kwa kutoa
matamko yaliyo nje ya Sera za Vyama vyao.
Amesema
kipengele cha 2.1 (m) cha Maadili ya Uchaguzi kinachoeleza Wajibu wa
Vyama vya Siasa na Wagombea katika kuendesha shughuli za Siasa wakati wa
Kampeni kinavitaka Vyama vya Siasa, Wagombea na Wafuasi wao kufanya
kampeni kwa kuzingatia misingi inayolenga kutangaza Sera ambazo
hazijengi chuki, mafarakano na kuleta mgawanyiko katika jamii.
“Katika
Kampeni zinazoendelea, baadhi ya vyama vya Siasa vimeanza kukiuka
taratibu za kampeni na maadili na kutumia fursa ya kampeni vibaya,
vinawasema viongozi wa Kitaifa , kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya
kumnadi mgombea na kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” Amesema Jaji
Hamid.
Amesema
kuwa vyama Vyama au Wagombea watakaoendelea kukiuka Maadili ya Uchaguzi
katika Mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya
Tanzania pamoja na Jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.
Jaji
Hamid ameeleza kuwa kipengele cha 5.3 cha Maadili ya Uchaguzi kinaeleza
wazi kuwa Chama au Mgombea atakayekiuka Maadili ya uchaguzi katika
jimbo au Kata yenye uchaguzi mdogo atafikishwa katika kamati ya maadili
ya ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki.
Aidha,
kipengele cha 5.10 cha Maadili ya Uchaguzi yaliyokubaliwa na Vyama
vyote vya Siasa kinafafanua kuwa Kamati za Maadili ya uchaguzi ngazi ya
Taifa, Jimbo na Kata katika kushughulikia malalamiko na kutoa adhabu
zinaweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukitaka Chama au
Mgombea kusahihisha kosa au makosa au kuomba msamaha hadharani.
Hatua
nyingine ni Kukisimamisha Chama au Mgombea kuendelea kufanya kampeni za
Uchaguzi, kutoza Faini, Kutangaza jina la Chama au Mgombea aliyekiuka
Maadili kwa kueleza kosa au Makosa yake kupitia redio, televisheni,
magazeti na njia nyingine za mawasiliano.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment