Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Maendeleo
ya nchi yoyote yanategemea nguvu kazi ambayo kwa asilimia kubwa
inatokana na vijana walioelimishwa na kupatiwa stadi mbalimbali za
kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
Serikali
inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha vijana wanapata ajira na
wengine kujiajiri kwa kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za kujenga
viwanda, kuanzisha miradi ya kuwapatia wenzao ajira ikiwemo ya kilimo,
mifugo, biashara ndogondogo pamoja na ujasiriamali.
Sio
kazi ya Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha vijana
wanapatiwa elimu na mafunzo ya kutosha ili waweze kujiajiri au kuajiriwa
na hatimaye kupunguza utegemezi.
Hivyo
Mashirika na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinatakiwa
kuhakikisha zinashirikiana na Serikali katika kuwapatia vijana ajira na
elimu ya kujitegemea kwani ukuzaji wa ajira kwa vijana ndio kipaumbele
kikubwa.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony
Mavunde anasema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kukuza ujuzi
wa nguvu kazi kwa vijana ambao utatolewa kupitia programu maalum ya
mafunzo kazini kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship), mafunzo kwa
vitendo kwa wahitimu (Internships) pamoja na urasimishaji wa ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi (Recognition of Prior Learning).
Mhe.
Mavunde anakakaririwa akisema kuwa, “Serikali yetu imetoa kipaumbele
cha juu katika kujenga ujuzi wa nguvu kazi, takribani vijana 15,000
watafaidika na programu hiyo kwa mwaka huu wa fedha kwani tayari
tumeanza kutekeleza kwa kuingia mikataba na Makampuni ya kutoa mafunzo
kwa vitendo katika maeneo ya kazi”.
Kwa
upande wa Mashirika, Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Plan
International limejitolea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia
vijana nchini kujiwezesha kiuchumi kwa kuratibu Mradi wa Uwezeshaji
Vijana Kiuchumi (YEE) ambao unawapa fursa vijana wanaoishi katika
mazingira magumu kuchangamkia fursa za elimu ya ufundi zinazotolewa na
Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA).
Mradi
huo wa miaka mitatu unafanyika katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro,
Pwani na Dar es Salaam, unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya
VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku
ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja
wa Nchi za Ulaya (EU).
Meneja
wa Mradi huo, Bw. Simon Ndembeka anasema kuwa mradi una lengo la
kuwasaidia vijana wapatao 9100 ambapo asilimia 53 wakiwa wakike kupata
elimu ya ufundi katika fani mbalimbali ambapo nia na madhumuni ikiwa ni
kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na kuendesha maisha yao ili kupunguza kasi ya umasikini nchini.
“Mradi
huu umelenga vijana wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanatamani
kujiendeleza kielimu lakini hawana uwezo huo hivyo tunawasihi vijana
mchangamkie fursa iliyotolewa kupitia shirika letu ili muweze kuendeleza
maisha yenu”, alisema Ndembeka.
Naye
Naibu Mkurugenzi wa Plan International-Tanzania, Bi. Gwynneth Wong
amesema kuwa mradi umeokoa vijana wengi kutoka katika mazingira
hatarishi na kuwafanya wawe na uwezo wa kujitegemea kwa kujishughulisha
na biashara mbalimbali za halali.
Ameongeza
kuwa asilimia 65 ya vijana 1225 waliohitimu mafunzo hayo wameajiriwa na
wengine wamejiajiri hivyo inaonyesha dhahiri kuwa miradi hii ya
kuwainua vijana kiuchumi inaleta mafanikio makubwa kwa vijana na taifa
kiujumla.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mradi wa YEE Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah
amesema kuwa mradi huo hautoishia kuwapatia ujuzi tu bali utaendelea
kuwawezesha kichumi ili kuhakikisha vijana hao wanasimama imara na
wanapata maendeleo kupitia fani walizozisomea.
“Shirika
la Plan International tumeamua kusaidia vijana kwa hali na mali hivyo
ni lazima kuhakikisha wanayafikia malengo yao, kwa sasa tumewasiliana na
VETA wafanye tathmini ya vifaa vinavyotakiwa na vijana hao ili tuweze
kuvinunua na kuwagawia waendeleze fani zao zinazowasaidia katika maisha
yao ya kila siku”, alisema Jeremiah.
Naye
Mkuu wa Chuo cha VETA - Pwani, Joseph Deusdedit amesema kuwa kadri
mradi unavyoendelea ndivyo wavyozidi kutoa nafasi nyingi za vijana
kupata elimu ya ufundi katika chuo hicho pia wameendelea kuwatengea
sehemu za kupata mafunzo zilizo karibu na maeneo wanayoishi kwa ajili ya
kuwawezesha kutambua kiurahisi fursa zilizopo katika maeneo
yanayowazunguka pia kuwapunguzia gharama za usafiri.
“Nitajitahidi
kushauriana na wadau wengine kufanya elimu hii ya vijana wanaoishi
kwenye mazingira magumu kuwa endelevu hata kama mradi hautoendelea kwa
sababu mradi huo umeonyesha mafanikio na unalenga vijana wa aina zote
wakiwemo walemavu, waliosoma na wasiosoma hivyo kuondoa adha kubwa ya
utegemezi katika familia zao,” alisema Deusdedit.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Future World, Robert
Mkolla amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ambao ndio asilimia
kubwa ya watanzania ni janga kubwa kiuchumi na kiusalama kwani vitendo
vingi viovu vinafanywa na vijana wasio na kazi za kuwaingizia vipato
hivyo shirika la Plan limeokoa vijana wengi katika matatizo ya namna
hiyo.
Mbali
na kupewa mafunzo ya elimu ya ufundi, Shirika la Uhamasishaji Hifadhi
Kisarawe (UHIKI) linatoa mafunzo ya kuweka na kukopa fedha kwa vijana
waliohitimu mafunzo ya ufundi chini ya mradi YEE ili kuwaelimisha jinsi
ya kutunza fedha zao.
Afisa
Msimamizi wa Miradi ya Kuweka na Kukopa – Kisarawe, Vuai Shame anasema
kuwa kuna umuhimu wa vijana kupata elimu juu ya utunzaji wa fedha pamoja
na upatikanaji wa mikopo ili waweze kuimarisha biashara zao na kuona
faida inayopatikana kutokana na biashara hizo.
“Kazi
ya UHIKI ni kuwasimamia vijana ili waweze kuunda vikundi vya kuweka na
kukopa fedha zitakazowasaidia kuendeleza biashara zao, mpaka sasa
tumefanikiwa kuwa na vikundi 27 vya vijana vilivyopo katika kata 4 za
wilaya yetu lakini bado tunaendelea kuwahamasisha vijana wengine kufanya
hivyo kwani vikundi vina faida”, alisema Shame.
Mradi
huu unaendelea kuwasaidia vijana wengi na umeonesha manufaa makubwa kwa
jamii kiasi kwamba Serikali inatambua mchango wao wa hali na mali.
Afisa
Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Yahaya
Mbogolume anasema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka kwani umekuwa
chachu ya maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya
wakazi wa eneo hilo ni vijana ambao walikuwa hawana cha kufanya lakini
kupitia fursa hiyo vijana wameweza kujiajiri.
Nae
Afisa Maendeleo ya Jamii – Kata ya Vingunguti, Pius Majura anasema
kuwa, Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupunguza utegemezi kwa
kuwasaidia vijana na wanawake kuweza kusimama wenyewe kwa kufanya
shughuli zao mbalimbali hivyo, mradi huo umewasaidia vijana wa eneo hilo
kuacha kufanya uhalifu na badala yake wamejikita katika shughuli za
halali ambazo zinawasaidia kupata kipato cha kuwawezesha kuendesha
maisha yao.
“Kabla
ya mradi huu kuanza vijana wengi walikuwa wakijihusisha na utumiaji wa
dawa za kulevya na wasichana wengi walikua wakifanya biashara za kuuza
miili yao, madanguro yalikuwa mengi lakini baada ya vijana kupatiwa
elimu na wengine kuweza kujiajiri na kuajiriwa, uhalifu umepungua kwa
asilimia kubwa”, alisema Majura.
Kwa
upande wake mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya mradi huo, George Geligoali
anatoa rai kwa vijana wenzie kuacha kudharau fursa zinazotolewa na
makampuni mbalimbali na badala yake wazichangamkie kwa kuwa fursa hizo
ni kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kiujumla.
Mhitimu
mwingine Rajabu Kilanga anasema kuwa mradi huo umemuwezesha kufahamu
jinsi ya kuhifadhi fedha kwa ajili ya maisha ya baadaye pia umemnufaisha
yeye pamoja na familia yake kwani kupitia fani ya umeme aliyoisomea
ameweza kupata tenda ndogo ndogo ambazo zinamsaidia kuyaendesha maisha
yake.
“Pamoja
na faida nyingi nilizozipata kupitia mradi huu lakini ukosefu wa ajira
za kudumu ni moja ya changamoto ambazo zinatukabili vijana tuliohitimu
mafunzo haya hivyo, tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia ajira ili na
sisi tuweze kutimiza malengo yetu na kuchangia katika kulijenga Taifa
letu”, alisema Kilanga.
Mradi
wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) -Tanzania, pia unashughulika na
kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata Elimu ya ufundi kwani
jamii bado haijatambua umuhimu wa kuwapatia elimu watu wenye ulemavu.
0 comments:
Post a Comment