TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Magufuli akutana na Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewashukuru Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa ushirikiano na mchango wao kwa
Serikali ya Tanzania ambao umesaidia kufikia malengo ya Serikali kwa mwaka
uliopita wa 2016. Rais Magufuli aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi waendelee
kuisaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea kwa mwaka 2017.
Mhe. Rais Magufuli ametoa shukrani
hizo leo wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya (Diplomatic Sherry Party)
iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam kati
yake, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais
Magufuli alisema kuwa mwaka 2016 ambao ulikuwa mwaka wake wa kwanza tangu
achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo nchi
imendelea kudumisha amani, mshikamano, umoja na Muungano umeimarika. Aidha
katika mwaka huo, Serikali imeongeza jitihada za kuimarisha demokrasia,
kupiga vita rushwa, ujangili na ufisadi.
Mhe. Rais Magufuli aliongeza
kusema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kiuchumi na kuwa nchi ya pili
yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika ikitanguliwa na Ivory Coast. Uchumi
wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia
7.2 mwaka jana kutoka asilimia 7.0
mwaka uliotangulia. Pia kiwango cha mfumuko wa bei kilipungua kutoka
asilimia 6.5 mwezi Januari 2016 hadi kufikia asilimia 2.5 mwezi Oktoba mwaka huohuo.
Akizungumzia suala la ukusanyaji
mapato, Mhe. Rais Magufuli alisema kwamba Serikali inasimamia kikamilifu suala
hilo ambapo kwa sasa kiwango cha ukusanyaji
wa mapato kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi
trilioni 1.2 kwa mwezi.
Kuhusu mpango wa maendeleo wa
miaka mitano 2016/2021, Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi hao kuwa, mpango huu
unalenga kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyoelekeza.
Alieleza kuwa katika kutekeleza
Mpango huo kiasi cha shilingi Trilioni 107 kinahitajika na kati ya hizo Serikali itatoa shilingi trilioni 59 ambazo
ni wastani wa shilingi trilioni 11.8 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo. Utekelezaji wa mpango huo umeshaanza ambapo Serikali katika Bajeti yake
ya mwaka 2016 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 29.5 ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti ya
Serikali kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo. Kiwango hicho ni cha juu zaidi
kuwahi kutengwa kwenye bajeti ya maendeleo katika historia ya Tanzania.
Fedha hizo zimeelekezwa kwenye
ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda kama vile
nishati, barabara, reli na maji. Aliongeza
kusema kuwa Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 5.5 zimetengwa kwa ajili ya
miundombinu ya usafirishaji na shilingi trilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya
nishati ya umeme. “Hii imetuwezesha kuendelea au
kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga,
maji pamoja na miradi ya umeme. Tuliweza pia kununua ndege mpya sita ambazo
bila shaka zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini”
Kwa muktadha huo, Rais Magufuli
aliwaomba Mabalozi kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika ujenzi wa Reli wa
kiwango cha kimataifa kutoka Dar Es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha
hadi nchi za Burundi, DRC na Rwanda. Serikali kwa kutumia fedha zake za ndani
itaanza kujenga kilomita 300 kuanzia Dar
Es Salaam hadi Morogoro.
Vile vile, Serikali imeweka
kipaumbele kwenye kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu iliyotengewa
trilioni 4.8 na sekta ya afya kiasi cha
trilioni 1.9. Kupitia mpango huu wa kuboresha sekta ya elimu, kiwango cha
udahili kwa watoto wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza na wale
wanaopokea ufadhili wa masomo ya juu kimeongezeka mara dufu ikilinganishwa na
miaka iliyopita.
Akizungumzia masuala ya
Diplomasia, Mhe. Rais Magufuli aliwaeleza Mabalozi na Wawakilishi hao wa
Mashirika ya Kimatifa kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi ningine
yameimarika ambapo Viongozi Wakuu kutoka
nchi mbalimbali wamefanya ziara nchini Tanzania. Aidha, yeye binafsi, Makamu wa
Rais, Waziri Mkuu na Viongozi wengine Serikalini wamefanya ziara za kuimarisha
ushirikiano kwenye nchi mbalimbali. Katika ziara hizo, Tanzania imesaini
mikataba mbalimbali ya ushirikiano. Mhe. Rais aliahidi kuwa Tanzania itaendelea
kuwa mwanachama mwaminifu kwenye Mashirika ya Kimataifa na Kikanda ikiwemo
Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya
Afrika Mashariki na mengine.
“Tunawashukuru sana Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda kwa kazi nzuri mnayoifanya
hapa nchini kwetu. Mafanikio yote haya niliyoainisha yamewezeshwa na
ushirikiano wenu na naahidi Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwenu ili muweze
kufanya kazi zenu vizuri” alisema Rais Magufuli.
Vilevile aliwaomba Mabalozi hao
kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuiwezesha kufikia malengo yake na aliwakaribisha
wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa za malighafi, nguvukazi na
soko kubwa lililopo nchini.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli
alianisha changamoto zinazochangia kukwamisha jitihada mbalimbali za Serikali
ikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa
kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hii ili kuziwezesha jamii zetu
kufikia maendeleo na ustawi. Pia kupitia Mabalozi hao alizipongeza nchi
zilizoridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na kueleza kuwa
Tanzania imeanza mchakato wa kuridhia Mkataba huo tangu mwezi Aprili, 2016.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais
aliwaeleza rasmi Mabalozi hao azma ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu mjini
Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake na kuwaomba Mabalozi hao
nao waanze mchakato wa kuhamia Dodoma.
“Mwaka jana wakati nakabidhiwa
uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi niliahidi ndani ya miaka mitano Serikali
itahamia Dodoma. Tayari Waziri Mkuu na baadhi ya Wizara zipo Dodoma. Nawaomba
Mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma kwani Serikali imekwishatenga
viwanja kwa ajili yenu, alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa
Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Edzai Chimonyo
alisema kuwa anaipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli
kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyopiga katika
kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake. Alisema kuwa katika kipindi hiki
wameshuhudia uchumi ukikua, nidhamu katika utumishi wa umma, ukusanyaji wa mapato
kuongezeka, na kiwango cha mfumuko wa bei kupungua.
Aidha, aliongeza kuwa wanaunga
mkono mpango wa Serikali wa kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo Reli kwa vile kutawezesha
kukuza biashara na nchi jirani na mataifa mengine kwa ujumla. Pia alipongeza
jitihada za Serikali katika kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi ambayo ina mchango
mkubwa kwenye maendeleo na kupongeza juhudi za Tanzania kwenye usuluhishi wa
migogoro kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na kuitaja Tanzania kuwa ni Kisiwa cha
Amani.
Kuhusu Mabalozi kuhamia Dodoma,
Balozi Chimonyo alisema Jumuiya ya Mabalozi inaunga mkono wazo hilo na wapo tayari
kuhamia Dodoma kama ilivyopangwa.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dar es Salaam, 10 Februari, 2017
0 comments:
Post a Comment