Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili kuwa Tanzania ambayo yatakuwepo Zanzibar.
Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye ameyasema hayo leo
Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya jitihada
mbalimbali ambazo Tanzania inazichukua katika kukuza Lugha ya Kiswahili
katika ngazi ya Kimataifa.
Nape
amesema kuwa maamuzi hayo ya kuifanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya
Lugha ya Kiswahili yametokana na Tanzania kuzalisha walimu wengi wa
Kiswahili ambao wanatumika katika ngazi mbalimbali za elimu ndani na nje
ya nchi.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Anastazia Wambura amesema kuwa
Wizara hiyo kwa sasa inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vyombo
vya habari vinakuwa mawakala wa kulinda Lugha ya Kiswahili ambapo
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na
wadau wa Kiswahili limeendelea kuendesha semina, warsha, makongamano na
kutoa elimu inayohusu matumizi fasaha ya Lugha ya Kiswahili.
Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa Waandishi wa Habari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Lugha hiyo inaendelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya Lugha hiyo katika majukumu yao ya kila siku.
“Kutumia
zana kama vile Kamusi na vitabu vya miongozo ya uandishi pamoja na
kuhudhuria makongamano ya Kitaifa na ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili
inasaidia kuongeza ujuzi na uweledi wa Lugha ya Kiswahili,
kujua istilahi za kisayansi na kiteknolojia na hivyo kuandika na
kutangaza kazi bora na zenye maudhui lengwa kwa jamii na kuepuka
upotoshaji wa maneno ya Kiswahili usio wa lazima,” alifafanua Anastazia
Wambura.
Hata hivyo Wizara hiyo iko katika maandalizi ya Sera ya Lugha ambayo itabainisha majukumu ya Vyombo vya Habari katika matumizi na uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.
Mwisho...
0 comments:
Post a Comment