Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais
Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa anapenda
kuendelea kufanya shughuli zinazosaidia kuleta maendeleo kwa watu na
jamii.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa
akizindua Taasisi yake ya Jakaya Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete
Foundation) alisema kuwa kwa muda mrefu amekua akipenda na kujihusisha
na shughuli mbalimbali za maendeleo ya watu na hivyo Taasisi yake
itamsaidia katika kufikia malengo yake.
“Nimetumia
muda wangu kwa ajili ya maendeleo ya watu, baada ya shule,
nilikitumikia Chama cha Mapinduzi(CCM), nilitumikia Jeshi na baadae
Serikali, kwangu Taasisi hii imekuwa chombo kitakachonisaidia kuendeleza
maono yangu na kutimiza ndoto zangu katika kuendelea kusaidia watu”
alisema Dkt. Kikwete.
Akiizungumzia
taasisi hiyo Kikwete alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka
sehemu mbalimbali duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi
zao.
Ameongeza
kuwa Taasisi hiyo imejikita kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne,
maendeleo ya jamii hasa katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko
ya hali ya nchi na kilimo kwa wakulima wadogo.
Pia Taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto.
Maeneo
mengine ambayo Taasisi hiyo inajihusisha nayo ni ni elimu kwa vijana
ili kukuza vipaji vyao na kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa
kijinsia na namna ambavyo Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.
Aidha,
alisisitiza kuwa Taasisi yake itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi
mbalimbali ili kushirikiana kuwaletea maendeleo watanzania na watu
mbalimbali duniani.
Dkt.
Kikwete amewataja Wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni
Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza
Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa
Willium Mahalu Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Tabibu cha
Bugando.
Wengine
ni Balozi Mwanaidi Maajar aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini
Uingereza, Abubakar Bakhresa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni
ya Bakhresa, Genevieve Sangudi Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya
Kimataifa kutoka Marekani.
Pia
wapo Dato’ Sri Idris Jala, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini
Malyasia, Balozi Charles R. Stith aliyekuwa Balozi wa zamani wa
Marekani nchini Tanzania pamoja na Dkt. Carlos Lopes ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa
(UNITAR).
Taasisi
ya Maendeleo ya Jakaya Kikwete ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na
hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini kukutana tangu
kuanzishwa kwake.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment