Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » RAIS MAGUFULI APONGEZWA KWA KUWAJALI WANYONGE KATIKA HUDUMA ZA AFYA.

RAIS MAGUFULI APONGEZWA KWA KUWAJALI WANYONGE KATIKA HUDUMA ZA AFYA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na. Georgina Misama MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa moyo wake wa kujitoa na kuwajali wanyonge hasa wagonjwa wasiojiweza na wenye uhitaji  wa gharama za matibabu.
Hayo yamesemwa leo na Bi. Neema Mwita Wambura maarufu kama ‘Mgonjwa wa Magufuli’ wakati alipotembelewa na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwaajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata majeraha ya moto.
“Ninamshukuru sana Mhe. Rais Magufuli kwa msaada wake katika matibabu yangu. Hivi sasa mimi nina maendeleo makubwa, naweza kuongea, kula na hata kugeuza shingo yangu. Nitamuombea Rais Magufuli mpaka siku naingia kaburini, Mungu ambariki” anasema Neema.
Akisimulia mkasa uliompata Neema anasema kwamba alimwagiwa maji ya moto na mumewe baada ya kuchuma mahindi mawili (2) shambani bila ya ruhusa yake. Mumewe huyo alitoweka na ndugu za Neema walihofia kumchukua kwa kuogopa kudaiwa mahali iliyolipwa na mumewe kama taratibu za kumuoa.
“Hakuna ndugu yangu hata mmoja aliyejitokeza kunisaidia kipindi chote cha matibabu. Walihofia kama ningefariki ingempasa huyo ndugu kurudisha mahali ambayo mume wangu alitoa. Nilikuwa nasaidiwa na majirani tu, nilikata tamaa ya kuishi nilikuwa nasubiri siku yangu ya kufariki ifike,” anasimulia Neema.
Aidha, Neema anawashukuru watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wodi ya Mwaisela wakiwemo manesi na madaktari kwa upendo na msaada mkubwa waliompatia toka siku wanampokea katika hospitali hiyo mpaka sasa ambapo anatarajia kurudi nyumbani.
“Nawashauri watanzania wasisikilize maneno ya watu wanaolalamika kwamba Muhimbili huduma sio nzuri, si kweli,kwa muda wote niliokaa hapa nimepatiwa huduma nzuri, tena kwa upendo na upole”
Akielezea maendeleo ya afya ya Neema, Mkurugenzi wa Upasuaji ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji Dkt. Ibrahimu Mkoma amesema kwamba, Neema alipokelewa hospitalini hapo tarehe 06/07/2015 akitokea Mkoa wa Mara wilaya ya Musoma , Neema alikuwa na majeraha ya mwaka mmoja toka aunguzwe.
Mpaka sasa Neema ameshafanyiwa oparesheni tatu kwa nyakati tofauti, zilizohusisha kutengenisha baadhi ya viungo kwani shingo, kifua na mkono wa kushoto vilishikana. Halkadhalika ilibidi kutoa ngozi ya sehemu ya mwili ili kufunika sehemu zile zilizoathirika zaidi.
“Ni katika kipindi hicho cha matibabu, Mhe. Rais alimuona Neema na kuguswa na hali yake, ambapo aliamua kumsaidia mpaka hivi sasa mnavyomuona. Neema sasa amepona na ataweza kuihudumia familia yake vizuri”,  aliongeza Dkt. Mkoma.
Akiongelea Moyo wa kujali wanyonge alionao Rais JPM, Dkt. Mkoma anasema kwamba Rais anaongoza kwa mfano, hivyo watanzania hawana budi kujifunza moyo huo wa kujali na kusaidia wahitaji wakati wote kwenye jamii.
Aidha, Dkt. Mkama ametoa wito kwa wadau na taasisi zinazohusika katika kutoa elimu kwa umma hususan madhara ya vitendo vya kikatili kutoa elimu hiyo kwa kuzingatia sehemu zenye ukubwa wa tatizo hilo ili kumaliza kabisa majanga ya aina hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa