Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » TAMKO LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA AFRIKA

TAMKO LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA AFRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



TAMKO LA WN-OMR - MMZ BW. JANUARY Y. MAKAMBA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA AFRIKA TAREHE 3 MACHI, 2017
Ndugu Wananchi,
Tarehe 3 Machi kila mwaka watanzania wote huungana na nchi nyingine za Afrika katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Afrika, ambayo huadhimishwa barani Afrika  kila mwaka. Siku hii imetengwa kwa lengo la kukumbuka umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira barani Afrika. Azimio la kuadhimisha Siku hii lilipitishwa na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri wanaosimamia Mazingira wa nchi za Afrika kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini Mwaka 2002. Siku hii iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na kuenea kwa hali ya jangwa Afrika. Kuanzia wakati huo siku hii ilikuwa inaadhimishwa nchini Ethiopia kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika.
Ndugu Wananchi,
Kikao cha 12 cha Baraza la Mawaziri wa Mazingira (AMCEN) kiliamua kwamba maadhimisho ya siku hii yawe yanafanyika kikanda. Hivyo kuanzia mwaka 2009 maadhimisho ya siku  ya Mazingira Afrika yalianza kufanyika kikanda katika nchi za Afrika na ndipo, mwaka 2010 nchi yetu ikapata fursa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya  yaliyofanyika jijini Arusha.  
Aidha, Umoja wa Afrika kwa kutambua juhudi na kazi iliyofanywa na Prof. Wangari Maathai kutokana na mchango wa mwanamke huyu katika hifadhi ya mazingira na  kuwezesha wanawake katika usimamizi endelevu wa maliasili na mazingira kwa ujumla waliamua tarehe 3 Machi kila mwaka iwe pia ni siku ya kumkumbuka yake iende sambamba na maadhimisho ya siku ya Mazingira Afrika. Hivyo tangu mwaka 2012 maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yamekuwa yakienda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wangari Maathai ili kutambua mchango wake katika utunzaji wa Mazingira. Mwanamke huyu alipata Tuzo ya heshima ya Nobel Laureate's green legacy kutokana na juhudi alizofanya.   

Ndugu Wananchi,
Tunapoadhimisha siku hii tutafakari kwa kina changamoto mbalimbali zinazochangia uharibifu mkubwa wa Mazingira. Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame, uchafuzi wa mazingira, ongezeko kubwa la idadi ya watu, kuwepo kwa shughuli za kiuchumi zisizoendelevu ambazo husababisha uharibifu wa mazingira. Hali hizo husababisha ongezeko la joto, ongezeko la ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, ongezeko la magonjwa mbalimbali ya mlipuko, upotevu wa bioanuai, uhaba wa chakula na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko la umaskini kwa jamii. 

Ndugu Wananchi,
Tunafahamu kabisa hali ilivyo sasa katika maeneo mengi nchini kwamba majira ya mvua yamebadilika na kusababisha ukame. Hivyo, inabidi tuhakikishe tunavilinda vyanzo vya maji kwa gharama yoyote ile. Aidha, katika kuadhimisha maadhimisho haya, kila mmoja awawajibike ipasavyo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi yasiyoendelevu ya bioanuai na rasilimali zake. Hivyo kila mtu afanye shughuli za kiuchumi zisizoharibu mazingira ikiwa ni pamoja na  kutumia nyenzo za uvuvi endelevu, kutumia nishati jadidifu, majiko sanifu na banifu, nishati mbadala, kudhibiti uchafuzi, kupunguza uzalishaji wa taka na kusimamia ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha miji yetu inakuwa safi.

Ndugu wananchi,
Natoa wito kwa watanzania tuadhimishe Siku ya Mazingira ya Afrika kwa kuendeleza na kusisitiza kampeni ya usafi katika maeneno yetu. Aidha, ninawagiza wananchi wote kuanzia ngazi ya Kaya, Mitaa, vikiwemo vikundi vya watu binafsi kushiriki kwenye shughuli za usafi ili kuhifadhi mazingira yetu. Nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi kuanzia  ngazi ya kijiji hadi mkoa kutumia fursa hii kuhuisha Kamati za Mazingira ili ziweze kusimamia shughuli za utunzaji mazingira katika maeneo yao. Aidha, mikoa, halmashauri za wilaya, sekta zote, pamoja na taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali  na wananchi wote kwa ujumla kushiriki katika shughuli za hifadhi na usafi wa mazingira  wakati wote. 

Ndugu wananchi,
Katika kuadhimisha siku hii, natoa wito pia kwa viongozi na watendaji katika ngazi zote kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingirakwa kuzingatia  sheria ya Mazingira ya mwaka 2004  pamoja na Kanuni zake.  

Baada ya kusema hayo, nawatakieni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yenye ufanisi.

Asanteni kwa kunisikiliza.

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa