Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetayarisha hati 214 kwa
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliosalimisha ofa zao za umiliki wa
ardhi kwenye wizara hiyo ili waweze kumiliki ardhi hizo kihalali.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini humo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
juu ya mambo mbalimbali yanayohusu wizara hiyo.
Waziri
Lukuvi amesema kuwa ni rahisi kwa wananchi wenye umiliki wa ofa
kutapeliwa kuliko wakiwa na umiliki wenye hati ambazo ni halali hivyo
ili kuondoa changamoto hiyo wizara ilitoa muda kwa wananchi kupeleka ofa
hizo ili watayarishiwe hati halali.
“Kuwa
na umiliki halali wa ardhi ni jambo kubwa kwa usalama wa wananchi
wenyewe, nataka ifike siku Tanzania iwe haina mtu anayemiliki ardhi kwa
kutumia ofa kwa sababu sasa hivi wizara haitoi ofa, ofa hizo zilishakoma
siku nyingi,”alisema Lukuvi.
Ameongeza
kuwa ingawa muda wa kusalimisha ofa hizo za umiliki umekwisha lakini
wizara hiyo inatoa muda zaidi kwa watu ambao bado hawajapeleka ofa zao
katika Halmashauri zao za wilaya kupeleka ofa hizo ili waweze kumiliki
ardhi hizo kwa hati.
Aidha,
akiongelea kuhusu utayarishaji wa teknolojia itakayohusika na masuala
yote ya ardhi inayojulikana kama ‘Mfumo Unganishi wa Ardhi’, Waziri
Lukuvi amesema kuwa tayari Kampuni ya Kifaransa iliyoshinda tenda
inaendelea na kazi na mnamo Julai mosi mwaka huu hati ya kwanza ya
kielektroniki ya mfano itatolewa.
Tayari
jengo litakalotumika kwa ajili ya shughuli hizo limeshakamilika na
mfumo huo bado unaendelea kutengenezwa ili kuwezesha wananchi wote
wanaomiliki ardhi Tanzania wanamilikishwa hati za kielektroniki.
0 comments:
Post a Comment