Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mtandao
wa Vikundi vya Wakulima nchini (MVIWATA) umeiomba Serikali kutunga
sheria ndogo ndogo zitakazowabana wafanyabiashara wa zao la ufuta ili
wakulima wapate faida ya uzalishaji wa zao hilo.
Maombi hayo yamebainishwa hivi karibuni na Afisa Masoko kutoka MVIWATA, Acquiline Wamba wakati wa warsha ya uboreshaji wa matumizi ya vipimo sahihi katika biashara ya mazao ya kilimo iliyofanyika mkoani Dodoma.
Bi.
Acquiline amesema Serikali inatakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa
kuweka sheria kali dhidi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwani Sheria
hizo zitawasaidia kuwapa maelekezo ya namna ya kuweka vipimo sahihi kwenye mazao ili kuongeza ushindani kwenye biashara.
“Wafanyabiashara
wasio waaminifu wamekua ni chanzo cha kukwamisha soko la nje kwa
kupeleka mazao yenye uchafu nje ya nchi, hii sio sahihi ndio maana
tunaomba Serikali itusaidie” alisema Bi. Acquiline.
Aliongeza
kuwa ili kuboresha soko la nje la zao la ufuta Serikali inatakiwa
kuhakikisha panakwepo na mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha mazao yanayoenda nje ni masafi.
Aidha,
Bi. Acquiline alifafanua kwamba kuwabana wafanyabiashara wa zao hilo
kutumia vipimo sahihi vya mizani itasaidia kukomesha wafanyabiashara
wanaowaibia wazalishaji hao kwani lengo halisi la kuweka mizani ni
kupunguza tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuongeza mchanga kwenye zao
la ufuta kwa lengo la kuongeza uzito.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Danford Chisomi
alisema kuwa Halmashauri bado haijawa na mizani ya mazao kutokana na
ufinyu wa bajeti hivyo aliahidi kushiriki katika kutatua changamoto
hizo.
“Halmashauri
itatafuta nafasi ya kuweka mizani pamoja na kuunda sheria mpya
ndogondogo za kuwadhibiti wafanyabiashara wa zao hilo”, alisema Chisomi.
Akiongea
katika warsha hiyo, mzalishaji wa ufuta Wilayani Bahi, Fikiri Bernard,
alisema kukosekana kwa mizani katika Halmashauri hiyo kunaathiri moja
kwa moja jitihada za wazalishaji pamoja na kusababisha upotevu wa mapato
kwa halmashauri hiyo.
“Vipimo
vingi vinavyotumiwa na wafanyabiashara huwa haviko sahihi kwa sababu
havijahakikiwa na Mamlaka husika kwa matumizi ya biashara hivyo
wafanyabiashara wamekua wakitumia mwanya huo wa ukosefu wa mizani kuweka
vipimo vyao wenyewe vya kununulia zao la ufuta,” alisema Bernard.
Ameongeza
kuwa Halmashauri hiyo imekua ikipoteza mapato mengi kwa kushindwa
kukusanya ushuru kutokana na kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu
wanaopenyeza mazao yao bila kulipa ushuru.
Vile
vile, mkulima huyo ameiomba Halmashauri kutenga vituo mbalimbali vya
kupimia mazao kwa ajili ya kupata vipimo sahihi vya mazao ili kuepuka
kuwaibia wakulima.
0 comments:
Post a Comment