MFANYABIASHARA maarufu wa Tanzania ambaye ni bilionea kijana zaidi
barani Afrika, Mohammed `Mo’ Dewji anayemiliki kampuni ya
MohammedEnterprises Tanzania Limited (MeTL) Group, amepania kuiteka
Afrika Mashariki kibiashara.
Mbali ya kuwa amekwishawekeza katika nchi 12 Afrika, jicho la
uwekezaji la Dewji kwa sasa limelenga zaidi Afrika Mashariki, amesema
lina soko kubwa la wastani wa watu milioni 160, lakini pia lina fursa za
kila aina zinazoruhusu ukuaji kibiashara.
Akizungumza na HabariLEO, Dewji ambaye kampuni yake imejikita katika
sekta ya viwanda, kilimo, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa, uuzaji
nishati za bidhaa za petroli ambavyo kwa pamoja vimeifanya MeTL iwe
taasisi kubwa na ya kwanza binafsi, inayoongozwa kwa kutoa ajira nchini
kutokana na kuajiri watu 28,000, akisema penye nia pana njia. “Mipango
ni mingi, na ninaona mwanga mbele. Kufikia mwaka 2025, dhamira ni
kuifanya MeTL iwe na kuongeza mapato na kufikia Dola za Marekanibilioni 5
(Sh trilioni 10.05) kwa mwaka.
Na katika ajira, tunataka tuajiri watu 100,000,” anasema Dewji
(pichani) mwenye utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.14 (Sh trilioni
2.4). Amezitaja nchi alizokusudia kufanya uwekezaji mkubwa kuwa ni
Burundi, Rwanda na Uganda kwa upande wa Afrika Mashariki, lakini pia
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Msumbiji na Zambia.
“Kuwekeza katika nchi hizi tumeona kunalipa,” alisema Dewji ambaye
kampuni yake inauza chai katika mnada wa zao hilo Mombasa huku akisema
wanatarajia pia kujenga kiwanda cha kusindika nafaka nchini humo.
Aidha, amesema MeTL inakusudia kujenga kiwanda cha nguo na sabuni ya
unga huko Ethiopia. Anasema viwanda vya nguo ni eneo muhimu la
uwekezaji, akitolea mfano nchi za Tanzania, Ethiopia, Zambia na Msumbiji
zenye pamba nyingi. “Lakini unahitaji umeme wa uhakika. Umeme ni ghali
sana, tunaangalia uwezekano wa kuzalisha umeme kwa ajili ya viwanda
vyetu vya nguo.
Nina uhakika hili linawezekana Tanzania na Msumbiji, angalau kwa
kuanzia kwa sababu tayari kuna gesi,” anasema bilionea huyo. Aidha, kwa
Tanzania, amesema anakusudia kuongeza vituo vya usambazaji wa bidhaa za
kampuni hiyo, kwa sasa akisema vipo zaidi ya 100 na magari zaidi ya
2,000. “Tuna mtandao mpana wa usambazaji nchi nzima pengine kuliko
kampuni nyingine yoyote,” alisema na kuongeza kuwa, miundombinu ya
usafirishaji ikiboreshwa, lakini pia huduma katika Bandari ya Dar es
Salaam zikiendelea kuboreshwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutimiza ndoto
za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania ipige hatua kwa kasi kuelekea
uchumi wa kati.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment