Imeandikwa na Mwani Aeshi
JESHI la Polisi linaendelea na kazi ya kuwaondoa wapiga debe katika
vituo mbalimbali vya mabasi ili kupunguza uhalifu unaotokea katika Jiji
la Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana jijini Dares Salaam na Kaimu Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya aliyeeleza kuwa
wanaendelea na kazi ya kuwafukuza wapiga debe katika vituo vya mabasi
ili kupunguza kero za wananchi wanazozipata kutokana na uhalifu
uliokithiri katika maeneo hayo.
Kamanda Mkondya alisema kazi hiyo itafanyika ndani ya wiki moja na
kutolewa ripoti kama imefanikiwa kudhibiti hali hiyo na baada ya hapo
itakuwa ni endelevu ili kukomesha wahalifu wanaotokana na wapiga debe
katika vituo vya mabasi jijini Dar es Salaam.
“Hatuwezi tukakaa kimya kuona vitendo vya uhalifu vinazidi kuendelea
katika Jiji la Dar es Salaam watu wanaibiwa vitambulisho vya benki,
vitambulisho vya shule, kuchaniwa nguo na mambo mengine mengi,” alieleza
Mkondya.
Hata hivyo, baadhi ya madereva wamesifu juhudi zinazofanywa na Jeshi
la Polisi za kuwaondoa wapiga debe katika vituo vya mabasi na kusema
kuwa hali hiyo itawafanya wafanye kazi zao katika hali nzuri.
Akizungumza hayo, mmoja wa madereva Yonah Lema, katika kituo cha
mabasi Posta, alisema uamuzi uliochukuliwa na Jeshi la Polisi kudhibiti
wapiga debe na kupunguza vitendo vya uhalifu ni jambo la kutiliwa mkazo
sana ili kufanya Jiji la Dar es Salaam kuwa na amani
CHANZO HABARI ,LEO
0 comments:
Post a Comment