Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SUMAYE AAMUA KUMWACHIA MUNGU

SUMAYE AAMUA KUMWACHIA MUNGU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema kuchukuliwa kwa mashamba yake mawili na serikali ni kinyume cha sheria na kwamba anamuachia Mungu endapo mahakama haitatenda haki.
Sumaye aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waaandishi wa habari kuhusiana na kuchukuliwa kwa mashamba yake, na kusema vyombo vya dola vimeingiliwa, hivyo asipotendewa haki anamwachia Mungu ndiye mwenye maamuzi.

“Njia za haki na za kikatiba zimeingiliwa kwa kutumia mabavu ya dola, nimebakiwa na njia hii … ambayo itawafanya Watanzania wajue ukweli na hatimaye kumuachia Mungu atuamulie, maana yeye ndiye mwenye kujua ukweli na ndiye anayetenda haki,” alisema Sumaye.

Sumaye ambaye ni Mjumbe wa kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuchukuliwa mashamba hayo ni mashinikizo ya kisiasa na sio kweli kuwa mashamba hayo hayajaendelezwa kama inavyodaiwa, anayamiliki kihalali na anayalipia kodi kila mwaka.

“Shamba la Mabwepande lilivamiwa na wananchi nikawa nalalamika zaidi ya mwaka umepita ndipo serikali inanipatia notisi ya kulichukua kwa madai kuwa sijaliendeleza. Notisi inatolewa tayari shamba lishavamiwa na watu wamejenga na tayari limeshaendelezwa. Je, hilo pori linatokea wapi?” Alihoji Sumaye.

Alisema eneo la Mabwepande lenye ekari 33 ameliendeleza na halikuwa pori kama linavyodaiwa na mwaka 2007 serikali ilitoa tangazo la kulifanya eneo la Mbwepande kuwa ni eneo la mipango miji na kuzuia maendelezo yoyote hadi serikali itakapotoa utaratibu.

Alisema hawakuliendeleza kwa maana ya kujenga majengo, lakini waliliendeleza kwa kulima mpaka hapo watakapopatiwa taratibu kamili za mipango miji ya matumizi ya eneo hilo, kama ilivyo kwa maeneo mengine na alikuwa amejipanga kupata wabia kwa ajili ya kujenga chuo kikuu.

“Mwaka 2015 wakati wa kampeni walishasema dawa yangu ni kuninyang’anya mashamba. Shamba hili na mengine tena ya viongozi wa CCM yalivamiwa na wavamizi tukatoa taarifa, lakini hakuna hatua ilichukuliwa ya kuwaondoa wavamizi hao,” alisema na kuongeza:

“Waliovamia kwenye mashamba ya wakubwa wengine waliondolewa kwa nguvu ya Jeshi la Polisi, lakini waliovamia kwenye shamba langu waliachwa.”

“Kwenye shamba la Mvomero sio kweli kuwa ni pori, kuna ekari 50 nimeweka mazao, ng’ombe zaidi ya 200, kondoo 300, nyumba zaidi ya mbili, umeme nimeweka, nimechimba visima viwili vya maji, kuna mabanda ya mifugo, ghala la kuhifadhi mazao na trekta hivi, hilo pori linatokea wapi ni vizuri serikali ikawa wazi kuwa wameninyang’anya kwa sababu za kisiasa,” alisema Sumaye.

Alisema shamba la Mvomero halikuwa kwenye orodha ya mashamba pori ambayo yalifanyiwa tathmini na yalitolewa maagizo kutoka ngazi ya juu kuwa shamba hilo linatakiwa kuingizwa katika idadi ya mashamba pori.

“Niliwajulisha kuwa kama wakitaka kuchukua shamba hilo labda watumie nguvu, lakini kisheria hamtaweza, kinachofanyika sasa ni kweli wameamua kutumia nguvu. 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, nilimwambia acheni kulipa visasi vya siasa kwa sababu mkivianzisha hata ninyi hamtakuwa salama, kwa bahati mbaya tahadhari niliyowapa imeangukia kwenye masikio yasiyosikia,” alisema.

Aidha, alisema aliamua kwenda mahakamani kufungua kesi kupinga dhamira ya serikali kufuta hati ya mashamba hayo na Mahakama Kuu imetoa zuio kutokuingiliwa na serikali hadi hapo shauri la msingi litakapoamuliwa.

Alisema kwa kutumia utawala wa sheria inayoijua, serikali imeamua kuyachukua mashamba hayo bila kujali kama kuna kesi na amri za mahakama dhidi ya hatua hiyo.

“Wiki iliyopita Agosti 14 Waziri Lukuvi alizungumza na vyombo vya habari akijaribu kuhalalisha kitendo cha serikali cha kuchukua mashamba 14 likiwamo shamba la mke wangu, Ester Sumaye. 

Nazungumzia mashamba ambayo yanahusu familia yangu kwa kuwa wameamua kulianzisha kulizungumzia jambo hili na mimi nimeamua kufanya hivyo, ili umma uelewe kile ambacho kinaendelea na wajue ukweli na hata dunia ijue kile kinachoendea Tanzania,” alisema.

Aidha, alisema vitendo anavyofanyiwa na serikali ni kutokana na uamuzi wake wa kuhamia upinzani na kamwe hatokatishwa tamaa na haitatokea akarudi CCM.
 Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa