WINGI wa watu uliojitokeza katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo
jijini Dar es Salaam jana, kuaga miili 13 ya Watanzania waliokufa kwenye
ajali ya gari nchini Uganda mapema wiki hii, ulisababisha eneo
lililotengwa la kuaga miili hiyo, kujaa na hadi wengine walilazimika
kuzuiliwa kuingia eneo hilo.
Watanzania hao wapoteza maisha kutokana na ajali ya iliyohusisha basi
dogo la kukodi aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T540 DLC
wakati wakitokea Kampala nchini Uganda, kuhudhuria harusi baina ya
daktari binti wa Kitanzania, Dk Annette Gregory Teu na mumewe, Dk
Treausuer Ibingira ambaye ni raia wa Uganda.
Bi harusi ambaye ni binti wa aliyekuwa Naibu Waziri katika Serikali
ya Awamu ya Nne, Dk Gregory Teu, pamoja na mumewe Dk Ibingira walikuwapo
jana msibani pamoja na ndugu wengine wa bwana harusi kutokea Uganda,
ambayo iliwakilishwa na Waziri anayeshughulikia Jiji la Kampala, Betty
Namisango.
Akizungumza kwa niaba serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi wa Rais
(Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angella Kairuki
alitoa salamu za rambirambi kwa niaba wa serikali na Watanzania kwa
ujumla, na kuzipa pole familia za wafiwa.
Kairuki alisema, “serikali imesikitishwa sana na ajali hii ambayo
imechukua maisha ya wenzetu 13 na tena kwa pamoja, tunawapa pole wote
ambao wamekutwa na msiba huu na tunawatakia safari njema mnapoenda
kuwapumzisha kwenye nyumba yao ya milele.”
Katika shughuli hiyo, pia walikuwapo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
John Kijazi, na mawaziri Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na
Uwekezaji) na Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria).
Wakati wa kuaga miili hiyo, vilio vilitawala huku karibu kila mmoja
akitaka kumuaga mpendwa wake, kutokana na wingi huo wa watu waliokuwa
wakitaka kuiaga miili hiyo, ilisababisha kuzuiliwa kwa watu wengine na
badala yake ndugu wa karibu tu na viongozi walipata wasaa wa kuaga.
Miili hiyo imesafirishwa kwenda katika mikoa mitatu ya Kilimanjaro,
Arusha na Dodoma wilayani Mpwapwa, ambako leo watazikwa. Dk Teu ni
mwenyeji wa Mpwapwa ambako alihudumu kwa miaka mitano kama mbunge
kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.
Miili hiyo iliwasili nchini juzi usiku kwa ndege na baada ya
kuwasili, ilipokelewa na wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) na kupelekwa moja kwa moja hadi Hospitali Kuu ya Jeshi
ya Lugalo, kupumzishwa kabla ya kuagwa jana asbuhi.
Waliopoteza maisha ni mtoto wa kwanza wa Naibu Waziri huyo wa zamani
aitwaye Sakazi, baba yake mzazi George Teu, baba mdogo wake, Mazengo
Teu, dada yake Rehema Teu, wadogo zake Esther Teu na Alfred Teu na
shangazi Paulina Ndagala.
Pia yupo shemeji wa Naibu Waziri huyo, Happy Soka, Bonny Njenga, kaka
wa Teu, Edwin Kimario, baba mdogo wake Vivian Mchaki, rafiki wa bi
harusi huyo, Aneth, Dk Eibnoth Laizer ambaye alikuwa ni mmoja wa wapambe
wa bibi harusi kwenye sherehe hiyo.
Majeruhi wanaoendelea na matibabu nchini Uganda ni mdogo wa Teu,
Erasto Teu, rafiki mwingine wa bi harusi, Dk Irene Lyatuu, mke wa
marehemu Njenga aitwaye Dativa Shayo na ndugu wa karibu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment