MSANII wa fi lamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ jana alianza
maisha mapya ya gerezani baada ya kuhukumiwa kifuko cha miaka miwili
jela. Makahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimhukumu Lulu kifungo hicho
baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji bila kukusudia ya aliyekuwa
mpenzi wake na msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa habari wa jeshi la Magereza
Mrakibu Msaidizi Lucas Mboje alisema Lulu amepokelewa kama wafungwa
wengine na adhabu yake alianza kuitumikia jana baada ya kufikishwa
gerezani.
“Lulu ni kama mfungwa mwingine yeyote, unapopelekwa gerezani
kutumikia kifungo hakuna suala la umaarufu, hatuangalii hilo…
anapokelewa kama wafungwa wengine, akifika anakabidhiwa mavazi yake na
kusomewa sheria na taratibu za kuishi gerezani lakini pia ana haki zake
za msingi kama kutembelewa na ndugu na jamaa na kukata rufaa kama ilivyo
kwa wafungwa wengine,” alisema.
Lulu amepata hukumu hiyo akiwa kwenye maandalizi ya kufanya filamu
yake baada ya kuwa kimya muda mrefu akisoma Stashahada ya Uongozi wa
Rasilimali Watu (HRM) katika Chuo cha Utumishi wa Uma (TPSC), Magogoni,
Dar es Salaam. Lakini pia ndiyo kwanza alikuwa amepata mkataba wa kuwa
balozi wa tuzo za filamu za SZIFF chini ya Azam kupitia chanel ya Sinema
Zetu.
Tuzo hizo zimepangwa kufanyika Aprili mwakani na tayari
zilishazinduliwa hivi karibuni. Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Sam
Rumanyika alisema ameridhika na ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa
mashitaka na maoni ya wa zee watatu wa baraza kuwa kweli Lulu aliua
bila ya kukusudia. Alisema kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa katika
Mahakama ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Aprili 12, 2012 kujibu mashitaka ya mauaji ya Kanumba.
Alieleza kuwa baada ya kusota rumande kwa takribani miezi kumi, Lulu
alibadilishiwa mashitaka na kushitakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia,
mashitaka yaliyomuwezesha kuwa nje kwa dhamana hadi jana aliposomewa
hukumu hiyo. Katika kesi hiyo, Lulu anadaiwa Aprili 7, 2012 maeneo ya
Sinza Vatican Dar es Salaam, alimuua bila ya kukusudia Kanumba na kwamba
upande wa serikali uliwakilishwa na Mawakili, Faraja George, Yusuph
Abood na Batilda Mushi huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Peter
Kibatala na Omary Msemo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema, kesi hiyo imejikita
katika ushahidi wa mazingira na kwamba mshitakiwa mwenyewe alikubali
kwamba yeye ndiyo alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemeu Kanumba ambaye
alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne. Alisema ili kuthibitisha kesi hiyo
ni watu wawili pekee ndiyo wenye uwezo huo ambao ni mshtakiwa na
marehemu Kanumba.
“Kwa sababu hiyo, mshitakiwa anatakiwa kutoa maelezo ya kina
yanayojitosheleza na akishindwa kufanya hivyo ataonekana kwamba yeye
ndiye muuaji. Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee
endapo utaendelea kumnyooshea kidole mshtakiwa,” alisema Jaji Rumanyika.
Alisema maelezo aliyoyatoa mshitakiwa yanakidhi viwango na vigezo kwa
kuwa alikubali kwamba walikuwa na mzozo uliosababisha kupigwa na kwamba
si matakwa ya sheria mshitakiwa athibitishe kosa la hasha, bali
anatakiwa kueleza namna kifo kilivyosababishwa. Alisema: “kwa maoni
yangu kuanguka au kudondoka kwa mtu mmojawapo katika ugomvi
inasababishwa na kusukumwa au kukabwa”.
Alisisitiza kuwa mshitakiwa alikuwa na jukumu la kutoa maelezo ya
kutosha kuhusu tukio lililotokea na kwamba alijikanganya wakati akitoa
utetezi wake. Alieleza kuwa Lulu aliiambia mahakama kwamba Kanumba
alikuwa amelewa na desturi ya mlevi mara nyingine huanguka, lakini yeye
alieleza kuwa aliburuzwa na kurudishwa chumbani hivyo kama alikuwa mlevi
hakueleza kama wakati wanakimbizana alianguka.
Pia alisema maelezo yaliyotolewa na Josephine Mushumbuzi kama
ushahidi wa upande wa utetezi, yanaacha maswali mengi kwa sababu hayana
hadhi ya cheti cha daktari kwa kuwa tayari mahakama ilitambulishwa kuwa
Daktari Paplas Kagaiga ndiyo daktari wa familia.
Alisema mshitakiwa mwenyewe pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco
ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo walieleza kuwa ndiye
daktari wa familia hivyo ndiye aliyepaswa kujua historia ya marehemu
ikiwemo afya yake na maradhi yanayomsumbua na siyo maelezo ya
Mushumbusi. Jaji Rumanyika alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa na
mahusiano ya kimapenzi kwa miezi minne na Kanumba, na kwa kuwa
alimfahamu kwa undani alitarajiwa ajue maradhi ya marehemu yanayomsibu
lakini kwenye utetezi wake hajaeleza.
“Maelezo yake yanakinzana na hekima ya kawaida kwa sababu hata pale
marehemu alipokuwa akimpiga na kumtishia kumuua kwa panga hakuthubutu
kufanya chochote, kumsukuma wala kumrudishia bali alichukua taratibu
zile za Kibiblia kwamba akupigaye shavu la kulia mgeuzie na la kushoto,”
alisema. “Akiwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hakutoa maelezo ya kina
na ya kutosheleza ni kitu gani hasa kilitokea hadi kukutwa na mauti,”
alisema.
Jaji Rumanyika alisema wakati tukio linatokea mshitakiwa alikuwa
mtoto wa umri wa miaka 17, lakini alikubali kuitwa mke na kuthubutu
kufanya vitu tofauti na maelekezo ya wazazi wake kwa kuamua kutoka
nyumbani kwenda matembezi usiku wa manane.
Alisema mtoto wa umri kama wake ambaye ameweza kuyafanya ya watu
wazima siyo mmoja wa wale watoto waliolengwa kulindwa na sheria ya
watoto, hivyo kuwa mtoto wa umri na kuweza kufanya kama alichofanya Lulu
kwa kujiamini, mahakama zitegemee kuona watu wazima wazee wakifanya
mambo ya watoto na kuomba kulindwa kwa haki sawa.
Alifafanua kuwa watunzi wa sheria ya watoto walikuwa na maana ya umri
na siyo ukomavu kama amesherehekea sikukuu ngapi za kuzaliwa na kwamba
kukua na kuzeeka ni jambo moja na ukomavu ni jambo lingine. “Kama
wanasheria na majaji wataendelea kuwa na fikra na mawazo yaliyosimama
huku jamii ikiwa inaendelea kwa kasi, basi watashindwa kuonesha kwa
vitendo utawala wa sheria kwa kasi hiyo nami sitaki kuwa wa kwanza,”
alisema.
Pia alisema mahakama ikiacha kufanya yale ambayo sheria hazijaruhusu,
lazima kuwepo na jamii isiyokuwa na maendeleo kisheria hivyo kushindwa
kutimiza matakwa ya kikatiba. “Ninajiridhisha kuwa kifo cha marehemu
kimetokana na ugomvi ndiyo maana mshitakiwa alishitakiwa kwa kosa la
mauaji bila kukusudia na hata katika utetezi wake, mshitakiwa alisema
marehemu alikuwa na wivu uliopitiliza ambao haukuwa na maana… lakini
hakuna mchezo usiokuwa na kanuni na katika mapenzi wivu ni moja ya
kanuni zake,” alisisitiza Jaji Rumanyika. Alisema, kuna wivu wa
maendeleo ambao huleta maendeleo lakini wivu wa mapenzi huleta
maangamizi.
Alieleza kuwa kama Lulu alishajiingiza katika mapenzi huku akifahamu
kwamba marehemu alikuwa na wivu kumbe hata alivyoanza kumshuku kwa simu,
alitakiwa aachane nayo ili kuepusha ugomvi lakini yeye alichukua kwa
misingi ya liwalo na liwe. Baada ya kutiwa hatiani, Lulu ambaye alikuwa
amevalia vazi aina ya dera na kujifunga kilemba kichwani alianza kukunja
kunja vidole na mikono yake huku akipandisha na kushusha gauni lake na
kuanza kujifuta machozi yaliyokuwa yakimtiririka.
Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Faraja alidai hawana
kumbukumbu za makosa ya nyuma ya Lulu, lakini kwa vile mashitaka hayo
yamehusisha uhai wa mtu, mahakama itoe adhabu stahiki dhidi ya
mshitakiwa. Wakili wa utetezi, Kibatala alidai mshitakiwa anategemewa na
familia yake ambao ni mama na mdogo wake, pia ni balozi wa taasisi
mbalimbali ambazo zinamuwezesha kiuchumi.
Pia alisema mshitakiwa huyo ataangaliwa kwa macho ya dhihaka na jamii
inayomzunguka na kwamba Lulu amebadilika tangu tukio lilipotokea, hivyo
anaamini ataendelea kubadilika kwani tayari alishakaa rumande. Alieleza
kuwa amemaliza masomo ya diploma na anategemea kujiunga na chuo kikuu
licha ya kwamba wazazi wake hawaishi pamoja bali wamekutana katika tukio
hilo.
“Marehemu alipaswa kumpa muongozo kwa wakati ule kwa kuwa alikuwa na
umri mdogo pia alipaswa kumsubiri. Hivyo mahakama ione adhabu ya kifungo
itamuathiri bali apewe nafasi ya kukaa nje ili aweze kuwa na
mawasiliano kati yake, jamii na walio karibu hivyo tunaomba asipewe
adhabu kali,” alidai Kibatala.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu ya Lulu, washitakiwa wengine watatu
ambao walisomewa hukumu jana na Jaji Rumanyika, waliachiwa huru kwa
mashitaka ya mauaji na hata baada ya Lulu kuhukumiwa kifungo hicho umati
wa watu waliofika mahakamani hapo ulihamaki na baadaye mama yake mzazi,
mashabiki, ndugu na jamaa zake waliangua vilio na kusababisha mama yake
Lulu kushikiliwa na watu watatu baada ya kukosa nguvu kwa kulia. Kwa
upande wa mama Kanumba, ambaye alitoa machozi akiwa nje ya mahakama
alishukuru mahakama kwa kutenda haki na kueleza kuwa anakwenda kumzika
rasmi mwanaye.
Aidha, Kibatala alidai kuwa upande wa utetezi umekusudia kukata rufaa
kupinga kifungo hicho. Lulu alizaliwa na kukulia Dar es Salaam na mama
Lucrecia Kalugira na baba Michael Kimemeta. Alianza kuigiza tangu akiwa
mdogo kwenye kundi la sanaa la Kaole.
Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Remnant Academy kabla ya
kwenda sekondari za Perfect Vision na St Mary’s, za Dar es Salaam.
Baadhi ya mafanikio katika sanaa ni kupata tuzo ya mwigizaji bora wa
Tamasha la filamu Tanzania (ZIFF) mwaka 2013 na tuzo ya Afrika Magic ya
Filamu Bora Afrika Mashariki mwaka 2016.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment