Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe.
Na Daniel Mbega
SHIRIKISHO la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limeanza zoezi la kukusanya taarifa na kuhakiki wanachama ili kuimrisha kanzidata yake.
Akizungumza na MaendeleoVijijini,
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza
Mwimbe, amesema zoezi hilo litarahisisha utendaji wa shirikisho katika
kuwafikia wanachama wake pamoja na kujua changamoto na vipaumbele ili
kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi.
“Tunahitaji
tupate idadi halisi ya wanachama wetu kwa sababu tunaamini kwa sasa
wameongezeka na hiyo itatusaidia kuweza kuwafikia kwa urahisi tukitambua
kila mwanachama anajishughulisha na nini, na nini changamoto zake
pamoja na vipaumbele,” alisema Mwimbe.
Mwimbe amesema kwamba, jukumu la TFC ni
kusimamia vyama vya ushirika, lakini katika wakati huu ambao taifa
linahitaji kujenga uchumi wake na kuongeza kipato cha kila Mtanzania ili
kufikia uchumi wa kati, ni vyema kutambua na kufuatilia kwa karibu
shughuli zinazofanywa na wanachama hao.
Amesema
asilimia zaidi ya 80 ya wanachama wao wanajihusisha na shughuli za
kilimo ambapo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za
ukame, pembejeo pamoja na masoko, hivyo kwa kuimaridha kanzidata yao
watakuwa na uwezo wa kutambua fursa na changamoto zilizopo katika maeneo
yote.
“Lazima
tuweke kumbukumbu sahihi, kwa sababu hii itasaidia, kwa kushirikiana na
wadau wengine wa maendeleo, kutafuta changamoto za wakulima pamoja na
kuwatafutia fursa, hasa za pembejeo na masoko.
“Kwa
kuwa tutakuwa na mawasiliano yote ya wanachama, tunakusudia
kuwaunganisha na masoko ya ndani na yale ya nje kupitia simu za
mkononi,” amesema Mwimbe.
Aidha,
amesema kwamba, kwa kuimarisha kumbukumbu hizo itawasaidia hata wao TFC
kutambua makisio ya uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa msimu.
“Kumbukumbu
hizi ni muhimu, tunaweza kuwa tunajua kwamba kwa msimu huu, mathalan
tumbaku limelimwa katika eneo lenye ukubwa gani na makisio ya mavuno ni
kiasi gani, vivyo hivyo kwa mazao mengine kama kahawa, pamba, mahindi,
mbaazi, ufuta, korosho na mengineyo.
“Kama
tukipata taarifa kutoka nje kwamba kuna watu au kampuni inahitaji tani
kadhaa za pamba ni rahisi kuwaunganisha wananchama wetu moja kwa moja na
kampuni hizo na wakauza kwa uhakika zaidi,” amesema.
Kuhusu TFC
TFC ndiye mrithi wa uliokuwa Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT) na
ilibadilishwa kufuatia sera mpya na kuanzishwa kwa Sheria mpya ya
Ushirika ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa mbadala wa Sheria ya Ushirika ya
mwaka 1991 iliyokuwa inaeleza kwamba vyama vya ushirika vilikuwa kama
sehemu ya vikundi vya kisiasa vya chama tawala.
Kwahiyo,
Sheria mpya ya Ushirika ya mwaka 2003 inaelezea tu usimamizi wa vyama
vya ushirika na wanachama wanastahili kuwa na sauti na ushiriki wa moja
kwa moja.
TFC
ni chombo kinachojitegemea kisichofungamana na upande wowote kikiwa
kinamilikiwa na wanachama wenyewe katika mukhtadha wa kufuata sheria na
kanuni za kimataifa za ushirika.
Kwahiyo,
TFC ni mwanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Ushirika (International
Co-operative Alliance - ICA), Shirikisho la Wakulima Afrika Mashariki
(East African Farmers Federation - EAFF), Shirikisho la Kimataifa la
Wazalishaji Bidhaa za Kilimo (International Federation of Agricultural
Producers - IFAP) na Committee of Artisanal and Workers Cooperatives
(CICOPA).
Kitaifa,
TFC ni mwanachama mwanzilishi wa Tanzania Private Sector Foundation
(TPSF) na Baraza la Kilimo Tanzania (Agricultural Council Tanzania -
ACT), zamani likijulikana kama Tanzania Chamber of Agriculture and
Livestock.
TFC
inashirikiana na wadau kadhaa wa kitaifa na kimataifa kama wizara za
Seriali, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo
(IFAD), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Muungano
wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Shirika la Maendeleo ya
Viwanda Vidogo (SIDO), na kadhalika.
Wanachama wa TFC
TFC ilisajiliwa rasmi Desemba 8, 1994 ikiwa na Hati ya Usajili Namba 5503 ambapo wanachama waanzilishi walikuwa 13 tu.
Pamoja na kwamba hivi sasa wanakusanya na kuhakiki taarifa kwa ajili ya kanzidata, MaendeleoVijijini inafahamu
kwamba, hadi kufikia mwaka 2015 TFC ilikuwa na vyama wanachama 3,339
Tanzania Bara vyenye wanachama mmoja mmoja zaidi ya milioni 1.5.
0 comments:
Post a Comment