TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema katika uchaguzi mdogo wa
madiwani utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu, katika kata 43 utagharimu
kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Aidha, tume hiyo imeteua wagombea 177 wa vyama mbalimbali waliochukua
fomu ya uteuzi namba 8C na fomu ya Maadili ya Uchaguzi namba 10, kati
yao 174 sawa na asilimia 92.7 ni wanaume na 13 sawa na asilimia 7.3
niwanawake.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema msingi wa
bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi
ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika. Alitoa mfano kwamba
kata yenye vituo 41, ina bajeti kubwa kuliko kata yenye vituo vikubwa.
Kailima alisema katika kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao
ni Msimamizi na Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa
kituo.
“Lakini pia kuna watu wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi
ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika
maeneo husika,” alifafanua. Alifafanua kuwa gharama nyingine za uchaguzi
ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka tume kwenda kwenye halmashauri
husika na kutoka halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi
unafanyika.
Gharama hizo pia zinahusu utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia
machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga Kura na maelekezo mbalimbali kwa
watendaji wa uchaguzi. “Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh
bilioni 2.5. Siyo kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi,
bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya
kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu
itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.
Tume pia imeviasa vyama vya siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo
wa madiwani kutekeleza Sheria ya Maadili ya Uchaguzi ya 2015
waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au mgombea atakayekiuka
maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye maadili hayo
ya uchaguzi. Alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuhakikisha
vinawaelimisha wafuasi, wapenzi na wanachama wao juu ya kutekeleza
maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni.
Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakiuka maadili
hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za
kinidhamu. Alitaja baadhi ya vitendo vya kuvunja maadili ya uchaguzi ni
kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya
kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.
Alisisitiza kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali
kwa chama au mgombea ambaye atakikuka maadili hayo. Alisema kamati hizo
zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 mara chama au mgombea
anapovunja maadili. Alizitaja baadhi ya adhabu zitazowakabili wagombea
au chama ambacho kitavunja maadili ya uchaguzi kuwa ni kuomba radhi
wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani wakati
wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea
kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka
maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000.
Kailima pia alisema chama cha siasa ambacho kinataka kufanya
mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe
msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo lazima lijadiliwe na vyama
vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi. Kuhusu vitambulisho mbadala
vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya
mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati
ya kusafirisha; Kailima alisema vitambulisho hivyo vitatumika tu kwa
watu ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.
Akizungumzia uteuzi uliofanywa na tume hiyo wa wagombea, Kailima
alisema jumla ya wanachama 155 sawa na asilimia 87.6 ya waliochukua fomu
za uteuzi, walizirejesha na kuteuliwa kuwa wagombea ambapo 145 sawa na
asilimia 93.6 ni wanaume na wagombea 10 sawa na asilimia 6.4 ni
wanawake.
Alisema hadi mwisho wa uteuzi ulipofika saa 10.00 jioni jumla ya
wanachama 22 sawa na asilimia 12.4 ya waliochukua fomu hawakuteuliwa
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutorudisha fomu, kurudisha fomu
nje ya muda uliotakiwa kisheria na fomu kutojazwa ipasavyo.
Vyama 13 vimesimamisha wagombea ambapo CCM imesimamisha wagombea 43
sawa na asilimia 100, ikifuatiwa na Chadema iliyosimamisha wagombea 43
sawa na asilimia 98, ACT-Wazalendo wagombea 18 sawa na asilimia 40 na
CUF wagombea 30 sawa na asilimia 70. Vyama vingine ni ADATADEA mgombea
mmoja (asilimia 2), ADC wanne (asilimia 7), CHAUMA mmoja (asilimia 2),
DP watatu (asilimia 5), NCCRMAGEUZI sita (asilimia16), NRA wawili
(asilimia 5), SAU wawili (asilimia 5), TLP mmoja (asilimia 2) na UDP
wawili (asilimia 5).
Aidha, alifafanua kuwa jumla ya wagombea 30 sawa na asilimia 19.4 ya
wagombea walioteuliwa waliwekewa pingamizi na wagombea wenzao na Msajili
wa Vyama vya Siasa kutokana na sababu mbalimbali. Kwa mujibu wa ratiba
ya uchaguzi, kampeni za uchaguzi tayari zimeanza na zitaendelea hadi
Novemba 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment