Imeandikwa na Hellen Mlacky
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amewatoa hofu Watanzania kwamba hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote
nchini, ambaye amegundulika au kuripotiwa kuwa na ugonjwa wa marburg
uliojitokeza katika nchi jirani ya Uganda tangu Oktoba 17, mwaka huu.
Akizungumza na wandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo jana jijini Dar
es Salaam, Ummy alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),
ugonjwa huo ni mkali na hatari kama ulivyo ebola, lakini umedhibitiwa.
“Ugonjwa huu ni mkali sana na hatari kama wa Ebola lakini umedhibitiwa
na WHO wameahidi kuendelea kutupatia taarifa kadri inavyowezekana...
Nawatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mgonjwa yeyote ambaye amegundulika
na ugonjwa huo hadi sasa,” alisema Ummy.
Aidha, alisema katika kuchukua tahadhari “tumeimarisha vituo vyetu
vya kuchunguza wananchi wote ambao wanaingia mipakani hasa katika mikoa
ambayo inapakana na Uganda ikiwemo Mara, Kagera na Mwanza.” “Ugonjwa huu
ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi
zinazosababisha kutokwa damu mwilini. Ugonjwa huu hauna tiba wala
chanjo,” alisema.
Dalili kuu za ugonjwa huo ambazo huanza ghafla ni pamoja na Homa
kali, maumivu makali ya kichwa pamoja na mwili kuishiwa nguvu ambapo
baadaye huambatana na kuharisha sana (majimaji), maumivu ya tumbo,
kichefuchefu na kutapika. Alisema dalili zingine za ugonjwa huo ni
kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa
na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayosababisha kifo kwa muda
mfupi.
Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku tatu hadi
tisa baada ya kupata maambukizi. Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana
na haraka kutoka mtu mmoja hadi mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na
mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji
mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa
ugonjwa wa marburg. Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa
nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg. TFDA yadhibiti dawa duni yaingiza
Maabara hamishika
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment