MATOKEO ya utafi ti wa Twaweza yameonesha kuwa asilimia 85 ya
wananchi wanaripoti kuwa, viwango vya rushwa vimepungua nchini kwa mwaka
2017 ikilinganishwa na mwaka 2014 ambao asilimia 78 walisema viwango
vya rushwa vilikuwa vikubwa kuliko miaka 10 iliyopita.
Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba, wananchi wameripoti kuwa
uzoefu wao wa kuombwa rushwa umepungua katika sekta zote mwaka huu
ikilinganishwa na 2014. Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jana jijini
Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema
matokeo hayo yametolewa kupitia utafiti uitwao: “Hawashikiki?
Mitazamo na maoni ya Watanzania juu ya Rushwa.” “Utafiti huu
unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani
Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.
Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa
1,705 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya Julai na Agosti
mwaka huu,” alibainisha Eyakuze.
Alisema matokeo hayo ya utafiti yanatia matumaini ikilinganishwa na
miaka mitatu iliyopita, ambako wananchi wamekuwa na mtazamo chanya
kuhusu mafanikio yanayojitokeza kutoka katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Sabina Seja alisema rushwa bado ipo na kuwataka wananchi na wadau
mbalimbali kutoa ushirikiano katika kupambana nayo badala ya kuiachia
serikali pekee.
Naye Ludovick Utouh aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), alisema ni kweli kwa kipindi hiki rushwa imepungua
tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka Watanzania kuichukia rushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema wananchi
wanaripoti kuombwa rushwa katika sekta mbalimbali kumepungua ambapo kwa
upande wa polisi ilikuwa asilimia 60 mwaka 2014 hadi asilimia 39 mwaka
2017, Ardhi asilimia 32 mwaka 2014 hadi asilimia 18 mwaka huu, Afya
asilimia 19 mwaka 2014 hadi asilimia 11 mwaka huu.
Kuhusu sekta ya maji, wananchi waliripoti kuombwa rushwa kwa asilimia
20 mwaka 2014 na kwa mwaka huu ni asilia sita, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) asilimia 25 mwaka 2014 na asilimia tano mwaka 2017, na
Asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ni asilimia 13 na asilimia sita kwa
mwaka huku.
“Sekta pekee ambayo rushwa iliripotiwa kubaki vilevile ni sekta ya
ajira ambapo asilimia 34 ya wananchi waliripoti kuombwa rushwa mwaka
2014, huku asilimia 36 wakiombwa rushwa mwaka 2017,” alieleza mtendaji
huyo wa Twaweza.
Alisema pengine kutokana na uzoefu wa viwango vikubwa vya rushwa,
wananchi wengi wamepata matumaini juu ya mapambano dhidi ya rushwa,
mwaka 2014 zaidi ya nusu ya wananchi ambao ni asilimia 51 walisema
rushwa haiwezi kupungua nchini, wakati mwaka 2017 asilimia 63 ya
wananchi wanasema itaweza kupunguzwa kwa kiwango fulani.
Alisema pamoja na mtazamo wa wananchi kwamba rushwa imepungua, sekta
za polisi na mahakama bado zinaongoza kwa rushwa, kwani asilimia 39 na
asilimia 36 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa mara ya mwisho
walipokutana na taasisi hizo mbili.
“Maelezo ya wananchi ya maana ya rushwa ni utoaji wa fedha wakati wa
kampeni asilimia 93, utoaji wa fedha na vitu kwa ajili ya kupata huduma
asilimia 78 na kuwalipa wafanyakazi hewa asilimia 65.
Asilimia 51 wanasema posho za vikao ni rushwa, lakini ni asilimia
tatu tu wanaosema wafanyabiashara kutoa fedha kusaidia kampeni za
uchaguzi na kisha kutarajia msaada ni rushwa,” aliongeza Eyakuze kuhusu
matokeo ya utafiti huo.
Aidha, alisema wananchi wengi wanataka wanaopatikana na hatia ya
rushwa wafungwe gerezani na adhabu hiyo ilichaguliwa zaidi kwa askari wa
barabarani aliyechukua rushwa ya Sh 20,000 asilimia 39, Ofisa Ardhi wa
Serikali za Mtaa anayechukua rushwa ya Sh milioni 5 asilimia 51 na
mwanasiasa mwandamizi wa Taifa aliyeiba Sh milioni 100 asilimia 49.
Kwa upande wa madai ya kashfa za rushwa za hivi karibuni, asilimia 84
ya wananchi wamesema serikali ilishughulikia kesi ya Acacia vizuri na
wananchi asilimia 67 walisema kesi ya TRA ya ukwepaji kodi
ilishughulikiwa vizuri, huku asilimia 38 wakisema kesi ya Escrow
ilishughulikiwa vizuri.
Hata hivyo, alisema wananchi wapo tayari kujitolea ili kupunguza
rushwa ambapo asilimia 81 walikubali kuwa ni muhimu kupambana na rushwa
hata kama itachelewesha maendeleo wakati asilimia 19 wanasema kusiwe na
ukali kwa kuwa itaathiri uchumi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment