Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imemuibukia kivingine, Askofu wa Kanisa la
Full Gosper Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, kuhusu utajiri
alionao ikisema haina muda wa kulumbana naye, bali inatekeleza maelekezo
ya Kamishna Mkuu.
Aidha,
mamlaka hiyo imesema haitaki kuwa kwenye malumbano na askofu huyo
wakati ikiendelea na uchunguzi dhidi ya vitega uchumi vyake na kuangalia
kama analipa kodi ya serikali.
Mkurugenzi
wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, jana alisema maofisa
wao wanaendelea kutekeleza tamko la Kamishna Mkuu wa TRA, Charles
Kichere, la kuchunguza utajiri wa Askofu Kakobe.
"Sisi
(TRA) hatutaki kuwa kwenye malumbano na Kakoke, tulichosema tumeishia
hapo. Alichosema Kamishna Mkuu tunaishia hapohapo, hatutakiwi
kujibishana naye," Kayombo alisema.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumamosi,
Kichere alisema mamlaka yake imeipokea kwa furaha kauli ya Askofu Kakobe
kuhusu utajiri wake na inataka kujiridhisha vyanzo vya utajiri huo.
Kichere
alisema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi, lakini
inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka
pekee.
Alisema wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za TRA.
Kauli
iliyoleta utata na kuibua uchunguzi huo ni ya Askofu Kakobe kukaririwa
wiki iliyopita akidai ana fedha nyingi kuliko serikali na anao uwezo wa
kumkopesha waziri pindi akiombwa kufanya hivyo.
Hata
hivyo, juzi ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza kufanya uchunguzi
dhidi yake, Askofu Kakobe alieleza historia ya maisha yake, mali za
kanisa na zake na misukosuko aliyopitia na kusisitiza kuwa tafsiri
iliyofanyika dhidi ya kauli yake kuhusu utajiri ni ya kimwili na siyo ya
kiroho. Alidai kauli yake ilimaanisha yeye ni tajiri wa kiroho na si
fedha.
Askofu
Kakobe aliishauri TRA kutohangaika naye, badala yake ikatafute fedha
mahali kwingine akieleza kuwa ana nyumba moja iliyopo Kijitonyama jijini
na aliijenga mwaka 1986 kwa gharama ya Sh. milioni mbili ikiwa ni
pamoja na gharama za kiwanja.
Huku
akishangiliwa na waumini wa kanisa lake kwenye ibada ya kuuaga mwaka
2017, Askofu Kakobe pia alidai kuwa mwaka 1995 alinunua gari aina ya
Nissan Patrol kwa kutumia sadaka za washirika wa kanisa na hivi karibuni
waliibuka watu waliochangishana na kumnunulia gari jingine.
Alidai
kuwa hata kwao Kakonko, Kigoma hajawahi kujenga hata choo na kilichopo
ni makaburi ya wazazi wake waliozikwa kwenye eneo la kuingia kwenye
nyumba iliyojengwa na wazazi wao.
Askofu
Kakobe pia alidai kuwa kanisa la FGBF ndani na nje ya nchi halina mradi
wowote wa kiuchumi kama shamba au hoteli na akasisitiza serikali
ichunguze kote huko.
Alibainisha
kuwa makusanyo yote ya sadaka huhifadhiwa kwenye akaunti iliyofunguliwa
mwaka 1990 katika Benki ya NBC na ni mali ya bodi ya wadhamini ambayo
imesajiliwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
0 comments:
Post a Comment