Hapa
nchini, tatizo la Saratani limekuwa likiongezeka kila mwaka. Shirika la
Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya wapatao
50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali Tanzania. Na kati ya
hao ni *wagonjwa 13,000 tu, sawa na 26% ndio wanaofanikiwa kufika katika
Hospitali zetu kuweza kupata matibabu*.
Aidha,
*wagonjwa walio wengi (takribani asilimia 70) hufika Hospitalini kwa
ajili ya matibabu wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa (hatua ya 3
na ya 4)*, hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kuweza kupona
maradhi hayo.
Takwimu za mwaka 2016/2017 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kwamba Saratani zinaoongoza nchini ni:
1. Saratani ya Kizazi (32.8%)
2. Matiti (12.9%)
3. Ngozi (Kaposis Sarcoma) (11.7%)
4. Kichwa na Shingo (7.6%)
5. Matezi (5.5%)
6. Damu (4.3%)
7. Kibofu cha Mkojo (3.2%)
8. Ngozi (Skin) (2.8%)
9. Macho (2.4%)
10. Tezi Dume (2.3%)
Katika
kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani *ninatoa wito na kuhimiza kila
mmoja wetu kupima ugonjwa wa Saratani. *Saratani inatibika endapo
itagunduliwa mapema*.
Serikali
ya Awamu ya 5 inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
itaendelea na jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi juu ya vyanzo
mbalimbali vinavyosababisha saratani ili kila mmoja wetu aweze
kujikinga. Vyanzo hivi ni pamoja na *Mtindo wa kimaisha (Life Style)
kama vile Uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa (kula vyakula
vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mboga mboga za kutosha),
matumizi ya pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya na kutofanya
mazoezi*.
Aidha,
Tutaongeza jitihada katika kuamsha ari na hamasa ya wananchi kupima
Saratani ili kujua hali zao sambamba na kusogeza huduma za uchunguzi na
matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani katika maeneo mbalimbali
nchini hasa vijijini.
Kwa
mwaka 2017, Serikali imeongeza Vituo 100 kutoka vituo 343 vilivyopo
awali kwa ajili ya huduma za kupima na matibabu ikiwa ni sehemu ya
jitihada zetu za kupambana na ugonjwa huu. vituo hivi (Zahanati, Vituo
vya Afya na Hospitali) tumevipatia vifaa Tiba na utaalamu ili kuwezesha
wanawake wengi kupima saratani ya Kizazi na Matiti pamoja na kupata
matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi papo hapo.
Tumelenga kuwafikia wanawake milioni 3 nchi nzima ifikapo Desemba 2018.
Vilevile,
Serikali inaendelea na jitihada za kusogeza huduma za matibabu ya
Saratani (matibabu kwa njia ya Dawa (Chemotherapy) na matibabu kwa njia
ya mionzi (Radiotherapy) katika Hospitali zetu za Rufaa za Kanda
(Mbeya, Bugando na KCMC). Pia tunaendelea kuimarisha huduma za matibabu
ya Saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwa kuweka mashine mbili mpya
za kisasa (Linear accerelators), ambazo zitasaidia kupunguza muda wa
kusubiri kwa wagonjwa kupata huduma za tiba ya mionzi sambamba na
kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100.
Kuanzia
mwezi April 2018, Serikali itaanza kutoa *chanjo ya kuwakinga wasichana
kupata ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi (HPV vaccine)*. Chanjo
hii itatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 - 14. Niwaombe wazazi
na walezi wenzangu tuwe tayari kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo
hii.
"Tunaweza, Ninaweza. Kwa Pamoja Tuwajibike Kupunguza Janga la Saratani Tanzania".!
Ummy Mwalimu, Mb
WAMJW
4 Februari 2018
0 comments:
Post a Comment