Tanzania yawa Mwenyeji ya Mkutano
wa Baraza la Wakimbizi Duniani
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ametoa wito kwa
Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Tanzania kutokana na mchango mkubwa wa
kuwahudumia wakimbizi ambao imekuwa ikiutoa kabla na baada ya uhuru, licha ya
uchumi mdogo ilio nao.
Waziri Mahiga ametoa wito
huo leo Jijini Dar Es Salaam katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani
(World Refugees Council-WRF) kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia jana kwenye
Hoteli ya Hyatt Regecy, Kilimanjaro.
Waziri Mahiga alieleza
kuwa Tanzania ilipokea wakimbizi kutoka Poland wakati wa vita ya pili ya dunia
na mwaka 1959 ilipokea wakimbizi kutoka nchi ya Rwanda. Aidha, baada ya uhuru,
Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi mara kwa mara na wakati wa mauaji ya
kimbari nchini Rwanda, Tanzania ilipokea wakimbizi wengi zaidi duniani.
Aliendelea kueleza kuwa
athari zinazotokana na kupokea wakimbizi wengi ni nyingi na kubwa hivyo, ni
jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuzisaidia nchi zenye wakimbizi wengi, hususan
zile zenya uchumi mdogo.
Katika kikao hicho, Waziri
Mahiga alitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania kujitoa katika
mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi duniani
(Comprehensive Refugees Response Framework – CRRF). Alisema katika mpango huo
wa CRRF, Serikali imesikitishwa na mapendekezo ya mpango huo ya kuitaka
Tanzania ikope fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi na
kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibika.
Halikadhalika, CRRF
inapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuwapa uraia, ajira na ardhi wakimbizi
wanaoingia nchini ili waweze kuwa huru na kujitegemea.
Alibainisha kuwa Serikali
ilishatoa uraia kwa wakimbizi zaidi ya laki moja na nusu. Jumuiya ya kimataifa
iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia makazi na huduma nyingine kwa
wakimbizi hao. Hata hivyo, Jumuiya ya Kimataifa haijatekeleza ahadi hiyo,
badala yake inaitaka Serikali ichukue mkopo wenye riba kwa ajili ya kuhudumia
wakimbizi.
“Misitu, ardhi, mazingira
na miundombimu mingine inaharibika kwa sababu ya wakimbizi, halafu tuchukue
mkopo na kulipa deni kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi, nadhani sio utaratibu
mzuri” Dkt. Mahiga alilalamika.
Dkt. Mahiga alieleza kuwa
amewasilisha ujumbe wa Serikali kwenye Baraza hilo ili lifikishe kilio cha
Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa kwa matumaini kuwa wao wanasikilizwa
zaidi.
Kwa upande wake, Rais
mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, alitoa maelezo kuhusu
dhamira ya kuanzishwa kwa WRC. Alisema WRC ilianzishwa mwaka 2017 kwa
ushirikiano kati ya Serikali ya Canada na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchi
hiyo. Lengo la chombo hicho ni kuangalia sababu zinazopelekea wakimbizi
kuongezeka, matatizo na changamoto
zinazowakabili wakimbizi na kutoa maoni ya namna ya kutatua tatizo la wakimbizi
duniani.
Baraza hilo linaongozwa na
jopo la watu wanne wenye uzoefu wa masuala ya wakimbizi duniani ambao ni Waziri
wa Mambo ya Nje wa zamani wa Canada ambaye ni Mwenyekiti, Mhe. Lyord Axworthy,
Mwenyekiti Mwenza ni Rais wa zamani wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, Makamu
Mwenyekiti ni Mwanadiplomasia wa zamani wa Canada, Mhe. Paul Heinbecker na
Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Pakistan ambaye pia ni Mwenyekiti
Mwenza, Mhe. Hina Jilani.
Baraza lilifanya kikao cha
kwanza Geneva, Uswisi mwezi Juni 2017 na baadaye kutembelea nchi za Jordan na
Ujerumani. Nchi hizo zimetembelewa kwa sababu Jordan ndio nchi inayopokea
wakimbizi wengi kwa sasa duniani na Ujerumani kutokana na kuruhusu kupokea
wakimbizi kulisababisha Serikali iliyopo madarakani kupata upinzani mkali
katika uchaguzi uliopita.
Kikao cha pili kinafanyika
Afrika na Tanzania imechaguliwa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya
wakimbizi. Aidha, kikao kijacho kitafanyika Bara la Asia katika nchi ya
Thailand na kitafuatiwa na kikao kitakachofanyika Bara la Amerika Kusini.
Katika kikao
kinachoendelea nchini, Nchi mbalimbali za Afrika zimealikwa zikiwemo Uganda,
Rwanda, Burundi, Kenya ambazo zieleza uzoefu wao kuhusu matatizo na sababu za
kutoa wakimbizi.
Baraza hilo linatarajiwa
kukamilisha ripoti yake mwaka 2018 na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa
ajili ya utekelezaji.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 13 Februari
2018
|
0 comments:
Post a Comment