Home » » TUME YA UCHAGUZI (NEC) YAJIBU UPOTOSHWAJI WA CHADEMA KUHUSU KUHAMISHA VITUO JIMBO LA KINONDONI

TUME YA UCHAGUZI (NEC) YAJIBU UPOTOSHWAJI WA CHADEMA KUHUSU KUHAMISHA VITUO JIMBO LA KINONDONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hussein Makame, NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema uamuzi wa kuhamisha vituo 46 vya kupigia kura katika jimbo la Kinondoni umezingatia matakwa ya kanuni za Uchaguzi kwa kuvishirikisha vyama vyote vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani jijini Dar es Salaam, kufuatia taarifa za upotoshaji zilizotolewa na baadhi ya magazeti zinazodai kuwa Chadema hakikushirikishwa katika uamuzi wa kuhamisha vituo hivyo.

Alisema kabla ya uamuzi wa kubadilisha vituo hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni iliitisha mkutano na vyama vya siasa tarehe 30 Januari, 2018 na wawakilishi 26 walishiriki kwenye mkutano huo wakiwemo wawakilishi wa Chadema.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyama vya siasa katika kikao kilichofanyika tarehe 30 mwezi Januari mwaka huu walikubaliana kuhamisha vituo 46 na katika vituo hivyo vituo 16 viko kata ya Kigogo, vituo 8 viko kwenye kata ya Mwananyamala na vituo 22 viko kwenye kata ya Kijitonyama” alisema Kailima.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifunga cha 21 (1) cha kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vituo vya kupigia kura havitakiwa kuwa kwenye maeneo ya watu binafsi, nyumba za mashabiki wa vyama vya siasa au maeneo ya majeshi na ibada.

“Nimesikitishwa na kauli ya Chadema eti hawakushirikishwa, nimesikitishwa kwa sababu kumbukumbu za mikutano zilizopo tarehe 30 Januari mwaka huu, chama cha Chadema kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Wilaya Bw. Mustafa Muro pamoja na Katibu wa Wilaya Bw. Shabani Kirita” alibainisha Kailima.

Alifafanua kuwa wawakilishi hao walihudhuria mkutano wa msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kinondoni na vyama vya siasa na katika mkutano huo kulikuwa na ajenda moja tu kuhusu kuhamisha vituo vya kupigia kura na vyama vyote kwa pamoja vilikubaliana kikiwemo Chadema.

“Unaposema chama cha Chadema hakikuhusishwa ninapata masikitiko makubwa sana.Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kuingilia mawasiliana ya ndani ya chama husika, kwa hiyo kama hakuna mawasiliano kati ya makao makuu na ngazi ya Wilaya hilo sio tatizo la Tume” alisema Kailima.

Alifafanua kuwa katika kata ya Kigogo kuna baadhi ya vituo vya kupigia kura vilikuwa ndani ya msikiti wa Kigogo na vingine vilikuwa ndani ya eneo la Zahanati eneo ambalo lilikuwa dogo kutosha kwa ajili vituo vya kupigia kura.

Kailima aliongeza kuwa, vituo 8 vya Mwananyamala vilikuwa kwenye eneo ambalo wananchi walikuwa wanalilalamikia, vyama vya siasa vikaridhia kwamba vituo hivyo vihamishwe na vituo 6 vikapelekwa kwenye kata inayohusika na vituo 2 vikapelekwa uwanja wa Kopa.

Akizungumzia vituo 22 kwenye kata ya Kijitonyama, Kailima alisema vyama vyote vilikubaliana kuvihamisha, hivyo Chadema kikisema havikukubaliana ndipo inapoleta shida.

Alisema Maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kipengele cha 9 (2) (C) kinasema kabla vituo vya kupigia kura havijahamishwa ni lazima Tume ishirikiane na vyama vya siasa na Tume imetimiza takwa hilo la kikanuni na vyama viliitwa vikakubali.

“Ukisema huwezi kuhamisha vituo kabla hujafanya Uboreshaji, huwezi kuacha makosa yakaendelea kuwa makosa.Hatujahamisha kutoa mkoa mmoja kwenda mwingine, bali tumehamisha kwa ridhaa na vyama vikaridhia.

“Kwa hiyo niwasihi chama cha Chadema kabla hakijaanza kulaumu wawasiliane na wenzao kwenye ngazi husika.” Alisema Kailima.

Katika hatua nyingine, Kailima amelisihi gazeti la Mwananchi, litoe habari sahihi kuhusu Tume na kuacha kuandika habari zinazoihusu Tume bila ya kuwasiliana nayo ‘kubalance’ kuhusu habari husika.

“Nalisihi gazeti la Mwananchi, tunaliheshimi ni gazeti bora na gazeti linaloheshimika, lakini nilisihi kabla halijatoa habari lazima lifanye balance ya habari” alisema Kailima na kuongeza kuwa:

“Wenyewe walipowauliza Chadema wakasema hawakushirikishwa walitatakiwa kuchukua fursa ya kuwauliza Tume kama hawakushirikishwa.

“Kwa hiyo nilisihi kwa sababu si mara moja wala mara mbili wamekuwa wakitoa taarifa ambazo si sahihi kuhusu Tume, tunawasihi na kuwaomba wanapotaka kutoa habari za Tume watoe habari za Tume zikiwa sahihi”

Alifafanua kuwa kulitaka gazeti hilo kwamba hata linapotaka kukosoa ni lazima likosoe kwa habari sahihi na sio kwa habari za upotoshaji na za upande mmoja.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa