Home » » YANGU MACHO JIMBO LA KINONDONI MAANA HUKU MTULIA...KULE MWALIMU

YANGU MACHO JIMBO LA KINONDONI MAANA HUKU MTULIA...KULE MWALIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Said Mwishehe

KWA heshima na taadhima, naomba nitumie nafasi hii kuwasalimia wananchi wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Natoa salamu zangu kwenu nikitambua kuwa pamoja na shughuli nyingine za ujenzi wa nchi yetu , pia mpo kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.Sababu za kufanyika za uchaguzi huo unatokana na uamuzi wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Maulid Mtulia kuamua kujiuzulu ubunge.Baada ya kujiuzulu akaondoka CUF na kujiunga CCM.

Sioni umuhimu wa kurudia sababu ambazo amezitoa Mtulia wakati anatangaza kujiondoa CUF.Hata hivyo moja ya sababu amedai alipokuwa CUF alijikuta akiwa kwenye wakati mgumu kutokana na mpasuko uliopo.Tunafahamu ndani ya CUF hakuko sawa kutokana na tofauti ya misimamo na mitazamo baina ya vingozi wa juu wa chama hicho.Hivyo Mtulia akaona bora ajiweke kando.Ndio sababu ambayo ameitoa.

Pia akasema juhudi za Rais ,Dk.John Magufuli za kuleta maendeleo zimemfanya aone haja ya kuunga mkono kwa kujiunga na CCM.Najua kila mtu anayo nafasi ya kuchambua na kupima anachosema Mtulia.Kwa sasa Mtulia anagombea tena ubunge wa Kinondoni kwa tiketi yaCCM.Kampeni zinaendelea Kinondoni na Mtulia ni miongoni mwa wanaomba kura kwa wananchi.
 
Katika uchaguzi huo ushindani upo kati ya Mtulia na mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema Salimu Mwalimu.Ni ushindani haswa na kila chama kilipozindua kampeni rasmi walitoa tambo nyingi.Tunasubiri mwisho wa tambo hizo utakuaje.

Kila mmoja anaamini ataibuka na ushindi.Chadema wanaamini Kinondoni ni ya Salumu Mwalimu na hivyo hivyo CCM nao wanaamini Kinondoni ni ya Mtulia.Sawa yupo mgombea wa TLP ,Dk.Godfrey Malisa ambaye naye anawania jimbo hilo.Najua wapiga kura ndio wenye kuamua nani awe mbunge wao baada ya kila mmoja kupita na kutoa sera za chama chake kuhusu nini watafanya kwenye jimbo hilo.

Pamoja na kwamba wananchi wa Kinondoni ndio wa kuamua bado ukweli uko pale pale wenye ushindani zaidi upo kwa Mtulia na Salum Mwalimu.Nikiri na kusisitiza wananchi wa Kinondoni wao ndio waaamuzi wa mwisho.Yangu macho tu na kueleza ninachoona kwa sasa.

Nikumbushe kidogo tu.Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,Mtulia aligombea Kinondoni na akashinda.Alishinda kwa sababu wananchi waliamini ni mtu sahihi kwao.Mtulia alipambana na Idd Azan (CCM) lakini akambwaga kwa wingi wa kura.Salum Mwalimu wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 aliamua kwenda kugombea jimbo la Kikwajuni visiwani Zanzibar.Hakushinda uchaguzi huo.

Hivyo tukiangalia uchaguzi mkuu uliopita utaona Mtulia alipewa imani na wananchi wa Kinondoni.Mwalimu hakuwa ameshinda kwa kule Kikwajuni.Sina maana atashindwa na uchaguzi huu maana mazingira ni tofauti na uchaguzi mkuu, lolote linaweza kutokea.

Hata hivyo kwa Salum Mwalimu yeye kugombea jimbo la Kinondoni, ndio mara yake ya kwanza.Sote tunafahamu kura ni siri ya mpiga kura hivyo anaweza kushinda Mwalimu au Mtulia ama Dk.Malisa.Kwa yoyote atakayeshinda hakuna dhambi, kikubwa inategemea wanachanga vipi karata zao katika kipindi hiki cha kampeni.Yangu macho.Wananchi wa Kinondoni ndio wataamua nani awe mbunge wao.Kupitia kampeni zinazoendelea watawafahamu wagombea wao vizuri na vyama vyao.

Sijui nikoje? Yaani kila nikiwaza uchaguzi huo naona ni vema nikatoa ushauri wangu kwa wananchi wa Kinondoni.Naamini ushauri wangu mtaukubali..Ila hata mkiukataa hakuna tatizo lakini nimeshauri tayari.Ni hivi naomba muwasikilize wagombea wote tena kwa umakini mkubwa.Wasikilizeni kila wanachosema na  kila wanachowaaahidi.Mwisho mtakuwa na nafasi ya kuamua nani atakuwa sahihi kwenu.

Huu si wakati wa kuchagua mbunge kama vile mpo kwenye ushindani wa Simba na Yanga.Uchaguzi mdogo unamaana kubwa licha ya kuitwa ni uchaguzi mdogo.Ni uchaguzi unaotokana na jimbo
kuwa wazi baada ya aliyekuwepo kuamua kujiuzulu kwa sababu ambazo amekuwa akizielezea.Hivyo kwa mujibu wa Katiba yetu lazima uchaguzi ufanyike.

Tayari Serikali iko madarakani na kila mwananchi anajua hilo.Hivyo kinachobaki ni kupata mbunge ambaye atakuwa mwakilishi wawananchi bungeni.Wanachagua mbunge atakayechukua changamoto za wananchi na kisha kuzipeleka kwenye vyombo vya mamlaka zipatiwe ufumbuzi wake.

Mnachagua mbunge ambaye atapinga kwa hoja na si kupinga hoja kwa vioja na vituko.Ni jukumu la wananchi wa Kinondoni kuamua kati ya Salumu Mwalim,Maulid Mtulia na Dk.Malisa nani mnaona mkimpa nafasi itakuwa rahisi kumtuma.

Wapo wanaosema fedha nyingi zinatumika kwenye uchaguzi huomdogo.Fedha ambazo zingeweza kutumika kwenye mambo mengine yakimaendelea.Wanaweza kuwa na hoja lakini ifahamike demokrasia nigharama  na haziepukiki.Zipo tu.Kama una bisha shauri yako.Ndio maana kote ambako wabunge walitangaza kuachia majimbo uchaguzi umefanyika tena.Si jambo jipya hata huko nyuma kumeshafanyika chaguzi ndogo mara nyingi tu.Unabisha nini?Huenda umesahau acha nikukumbushe uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga baada ya Rostam Aziz kuamua kujiuzulu.Ni moja tu ya mfano kati ya mingi.Fedha zilitumika kama ambavyo zinatumika sasa.

Hata ikitokea mbunge aliyepo amefariki lazima Tume ya Taifa Uchaguzi(NEC)itangaze kufanyika kwa uchaguzi mdogo.Huo ndio utaratibu iwe ni gharama kubwa au ndogo.Kwa wananchi wa Kinondoni kikubwa kwenu ni kuchekeka na kuwapima wagombea waliopo mbele yenu na kisha kupata mtu sahihi ambaye mtashirikisha naye kutatua kero zenu.

Tunafahamu uchaguzi huo wa Kinondoni kwa vyama vya upinzani ni kipimo cha wao kama bado wanaendelea kuaminika kwa wananchi au la.Na kwa CCM nao ni uchaguzi ambao wanautazama kwa jicho la aina yake.Ni uchaguzi ambao unatoa picha ya namna ambavyo wananchi wanawaamini kwa kiwango gani.

Kimsingi uchaguzi wa Kinondoni ni uchaguzi mdogo kama ambavyo tunaelezwa lakini umebeba sura ya kitaifa kutokana na mazingira yaliyopo.Nimalize tu kura zitakazopigwa siku ya uchaguzi zitatoa majibu ya nani anatakiwa na wananchi wa Kinondoni.Yangu macho maana huku namuona Mtulia na kule namuona Mwalimu.

TUWASILIANE 
0713833822

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa