Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MPOTO AKOSHWA NA PROGRAMU YA UMILIKISHAJI ARDHI WA WIZARA YA ARDHI CHINI

MPOTO AKOSHWA NA PROGRAMU YA UMILIKISHAJI ARDHI WA WIZARA YA ARDHI CHINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi , William Lukuvi akikabidhi hati kwa mmoja wazee waliofanikiwa kumilikishwa ardhi.
Waziri Lukuvi akutana na wananchi waliokabidiwa hati zao

Na Mwandishi wetu, Globu ya jamii.

MSANII wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto ambaye amekuwa kioo cha jamii kwa muda mrefu kutokana na kutoa nyimbo za kijamii zenye kuwataka wananchi kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato cha halali, kukemea rushwa na uonevu, Ijuma hii amefurahishwa na Programu ya Umilikishaji Ardhi (Land Tenure Support Programme - LTSP).

Programu hiyo ambayo inatakelezwa katika Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Waziri wake, Mhe. William Lukuvi  ili kukabiliana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiibuka katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Programu hii ni mahsusi kwa wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ambapo takribani vijiji 160 vitanufaika. Hadi sasa, Programu imehakiki na kupima vipande vya ardhi 84,795 katika vijiji 40 vya Wilaya za Kilombero na Ulanga. 

Kati ya vipande vilivyohakikiwa na kupimwa, jumla ya Hati za Hakimiliki ya Kimila 24,650 zimeandaliwa.

Mpoto ambaye amekuwa akitembea katika maeneo mbalimbali ya nchi kusoma mazingira na kuwasikiliza wananchi wanasema nini juu ya maisha yao ili anapoandika nyimbo zake ziwe na kero za wananchi ambazo amezishuhudia kwa macho yake, wiki hii alipita mkoani Morogoro na kuzungumza na wananchi kuhusu maisha yao ndipo lilipo ibuka suala la programu ya Umilikishaji Ardhi (Land Tenure Support Programme - LTSP).

Mshairi huyo amesema baada ya kuzungumza  na wananchi kadhaa ambao wamepitiwa na Programu hiyo aligundua nyuso zao jinsi zilivyokuwa na furaha baada ya kukabidhiwa hati zao ambazo zimeongeza thamani zaidi ya ardhi yao (viwanja na mashamba)  kwa kuwa tayari vinatambulika kisheria.

“Kwa miaka mingi nchi yetu imekua na migogoro ya ardhi kati ya mtu na mtu,kijiji na Kijiji, wakulima na wafugaji, hata wawekezaji na wana nchi, Wizara ya Ardhi kupitia Mpango wa Land Tenure Support Programme (LTSP) inayotekelezwa katika Wilaya Tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi baadae kusambazwa Nchi nzima imefanya kazi kubwa sana,” alisema Mrisho Mpoto.

“Binafsi kama kawaida yangu kuzunguka kila koja na nchi yangu na kuzungumza na wananchi, nimeona ukubwa wa hii Programu, imeona thamani ya hii programu, wananchi wanaongea kwa furaha ya hali ya juu kutokana na hii programu. Mimi sio msemaji wa serikali lakini wakati nikiwa katika harakati za kutembea kwa ajili ya shughuli zangu za sanaa huwa napata fursa ya kuongea na wananchi wa eneo husika, wakazi wa Morogoro wanaishukuru sana serikali pamoja na Waziri Lukuvi,  naamini hii programu inaweza kuwa mwarobaini wa haya matatizo ya ardhi, maana kila kipande cha ardhi kitapimwa na mwananchi kupewa hati yake ya umiliki, naamini itaweza kuondoa kabisa migogoro ya nrdhi nchini Tanzania, hongera Mhe.Lukuvi,” aliongeza Mpoto.

Alisema bado ataendelea kutembea katika maeno mbalimbali ya nchi kwa ajili ya kukutana na mashabiki wake wa muziki na kuzungumza nao kuhusu mambo mbalimbali ya nchi na pale ambako ataona kuna haja ya kutoa msaada atawasiliana wahusika kwaajili  ya kutatua kero za wananchi.

Kazi nyingine zilizotekelezwa na programu ya LTSP ni pamoja na kusimika alama za msingi 54 za mtandao wa kijiodesia katika Wilaya za Kilombero, Ulanga, Malinyi na Mufindi,  Kupima mipaka ya vijiji 121 na kutatua migogoro 71 ya mipaka ya vijiji iliyodumu kwa muda mrefu, Kuandaa vyeti vya Ardhi ya Kijiji kwa vijiji 57, Kuandaa mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji kwa vijiji 53 na Kuchangia katika ujenzi na ukarabati wa masjala za ardhi na ofisi za vijiji katika vijiji 61.

Viongozi wengi wa Wizara wanaitembelea programu hiyo mara kwa mara na uongozi wa Wilaya na wananchi wanatoa ushirikiano mkubwa sana kwa kuwa programu iko katika Wilaya zao.

Hivi karibuni Katibu Mkuu Bibi. Dorothy Mwanyika mara tu baada ya kuteuliwa na Mhe Rais kuwa Katibu Mkuu wa Wizara alitembelea programu hiyo na kujionea namna programu inavyotumia teknolojia ya kisasa kabisa kupima ardhi ya wananchi vijijini. Pia, Mhe Naibu Waziri Mhe. Angelina Mabula nae alifanya ziara katika eneo la programu.
CHANZO MICHUZI BLOG

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa