TAARIFA KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA
KIPINDUPINDU NCHINI KWA KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI 2018 ILIYOTOLEWA NA MHE.
UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO,
TAREHE 9 APRILI, 2018.
Ndugu Wanahabari,
Serikali kupitia Wizara ya
Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekuwa ikitoa taarifa ya
mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na hatua zinazochukuliwa
kudhibiti ugonjwa huu Kuanzia Januari hadi kufikia tarehe 31 Machi 2018, jumla
ya wagonjwa 1448, wametolewa taarifa, na
kati ya hao 27 wamepoteza maisha.
Kwa kipindi cha Januari wagonjwa 365 na vifo 9 walitolewa
taarifa, Februari wagonjwa 996 na vifo 18 na Machi wagonjwa 87 bila kifo.
Mwenendo wa takwimu hizi za ugonjwa wa Kipindupindu zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa
na vifo imepungua kwa kiasi kikubwa. Aidha, Mkoa wa Dodoma umeongoza kwa
kipindi cha Januari hadi Machi kwa kuripoti jumla ya wagonjwa 583 kati ya 1,448
walioripotiwa nchi nzima sawa na asilimia 40.3%, ikifuatiwa na Ruvuma 374
(25.8%), Rukwa 276 (19.1%), Iringa 88 (6.1%), Morogoro 56 (3.9%), Songwe 37
(2.6%), Kigoma 25 (1.7%) na Manyara 9 (0.6%).
Kwa mwezi Machi 2018, jumla ya wagonjwa 87 bila kifo
wametolewa taarifa, ambapo ni pungufu kubwa sawa na asilimia 91.3% ukilinganisha
na mwezi Februari 2018 ambapo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 996 na vifo 18. Kwa
mwezi Machi mikoa na halmashauri ambazo zimeendelea kutoa taarifa ya ugonjwa wa
Kipindupindu nchini ni Dodoma
(Mpwapwa-35, Chamwino-15, Dodoma Mjini-6, Kongwa-5), Ruvuma (Nyasa-18, Mbinga-5), Rukwa
(Sumbawanga Vijijini-5), na Iringa
(Kilolo-2).
Ukilinganisha idadi ya wagonjwa waliotolewa taarifa mwezi
Februari na ule wa mwezi Machi, mikoa imeweza kufanikiwa kudhibiti ugonjwa huu
kwa kiasi kikubwa. Mfano mkoa wa Morogoro umefanikiwa kudhibiti kikamilifu kutoka
wagonjwa 56 mwezi Februari na kutokuwa na wagonjwa wowote mwezi Machi. Mikoa
mingine iliyofanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa sehemu kubwa katika
kipindi cha mwezi mmoja ni Iringa (punguzo la asilimia 97.7%), Rukwa (punguzo
la asilimia 96.1%) na Ruvuma (punguzo la asilimia 92.7%). Mkoa wa Dodoma pia
umefanikiwa kupunguza idadi ya wagonjwa kwa takribani asilimia 83% katika kipindi
cha mwezi mmoja.
Wizara inatoa pongezi kwa Mikoa kwa jitihada mbalimbali
walizozichukuwa kudhibiti ugonjwa huo ambayo imepelekea kupunguza kwa sehemu
kubwa kuenea kwa ugonjwa huu katika kipindi cha mwezi wa Machi.
Ndugu Wanahabari,
Ingawa takwimu hizi zinaonyesha kuwa ugonjwa umepungua,
bado uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu na kupata maambukizi mapya
ni tishio hata kama ni Halmashauri moja tu itakuwa na wagonjwa wa Kipindupindu.
Tishio hili inaongezeka katika msimu huu wa mvua ambapo inaweza kuongeza kasi
ya kuenea kwa maambukizi ya Kipindupindu. Hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za
kuzuia ugonjwa huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki
inayotolewa.
Ni dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi mbalimbali
na jamii kwa ujumla ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa
Kipindupindu. Wizara inasisitiza kuwa
wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali za
kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye Halmashauri na Mikoa. Viongozi
wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha
jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Ndugu Wanahabari,
Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na
Halmashauri, Mikoa, hasa iliyotoa taarifa kipindi cha Januari hadi Machi,
pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu. Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na
usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
1.
Kujenga na kutumia vyoo
bora katika maeneo tunayoishi.
2.
Kunawa mikono kwa maji
yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na baada ya
kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
3.
Kunywa maji safi na
salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na
kupoa.
4.
Kuzingatia ushauri na
elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, ili jamii iondokane na imani
potofu kuhusu Kipindupindu.
5.
Kufikisha wagonjwa wa
Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
6.
Kutotiririsha
maji taka ovyo
Vile vile, Wizara inasisitiza yafuatayo yasimamiwe
kwenye Halmashauri na Mikoa yote nchini,
1.
Utoaji wa taarifa
sahihi za ugonjwa wa Kipindupindu na kwa wakati kwa kufuata miongozo iliyopo.
2.
Usimamizi wa
utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa ni pamoja na;
o Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za
usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
o Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara
za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
o Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya
usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
3.
Kuimarisha mifumo
ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na vijijini
hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
o Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa
kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
o Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia
klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji
ufanyike kulingana na miongozo.
Hitimisho
Wizara kwa ukaribu itaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa
wa Kipindupindu nchi nzima. Aidha, Wizara inawashukuru wadau wote wa sekta
mbalimbali, wataalamu na watumishi, waandishi wa habari na wananchi kwa
michango yao mbalimbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu
nchini.
Asanteni
sana
0 comments:
Post a Comment