Meneja wa NSSF Mkoa wa Kinondoni, Bw. Large Materu ametoa wito kwa wajasiriamali kuendelea kujiunga na kujiwekea akiba katika Mfuko ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya uzee, uzazi na matibabu.
Alitoa wito huo wakati akiongoza utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii kwa viongozi wa masoko na baadaye wafanyakazi wa NSSF waliweka kambi kwenye masoko ya Kawe na Tegeta Nyuki kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya, kuhamasisha uchangiaji ambapo hamasa ya wajasiriamali kupata elimu na kujiunga imekuwa kubwa.
“Napenda kutoa wito kwa wajasiriamali wote wakiwemo mama lishe, bodaboda, wakulima, wafugaji, wavuvi kuwa NSSF ndio Mfuko wao, hivyo waendelee kujiunga na kujiwekea akiba ili waweze kunufaika na mafao yote kama vile ya uzee, urithi, uzazi na matibabu,” alisema.
Bw. Materu alisema NSSF imeweka utaratibu mzuri wa wajasiriamali kujiunga na kuchangia ambapo mwanachama baada ya kujiandikisha anapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na anapaswa kuchangia kuanzia shilingi 30,000 au 52,200 au zaidi kwa mwezi na anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki au mwezi ili aweze kunufaika na mafao hayo.
Aidha, alisema NSSF imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma kwa wanachama na wananchi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ambayo inarahisisha huduma. "Tunaishukuru Menejimenti ya NSSF kwa kuweka nguvu kubwa sana katika kubadilisha mwelekeo wa utendaji kazi kuwa wa kidijitali zaidi ambapo imepelekea wanachama na wananchi kwa ujumla kupata huduma hukohuko waliko bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF," alisema Bw. Materu.
Alisema hayo ni mafanikio makubwa na kuwa lengo la NSSF ni kuendelea kufanya maboresho zaidi ya mifumo ili kumuwezesha mwanachama aweze kufungua madai ya mafao yake kwa njia ya mtandao bila ya kulazimika kufika kwenye ofisi za Mfuko.
0 comments:
Post a Comment