Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIMA AFYA ZAO KUELEKEA DESEMBA MOSI, 2015.‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wito umetolewa kwa wananchi kote nchini kuyatumia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka kupima afya zao ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema  Siku ya Ukimwi Duniani nchini itaadhimishwa kwa  kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi  kupima afya zao na kupata elimu ya kujikinga  na maambukizi ya ugonjwa huo.

Ameeleza kuwa  maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za Utoaji wa Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa VVU katika maeneo mbalimbali kote nchini kupitia vituo vitakavyowekwa, Kufungua kituo cha maarifa cha udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida ambayo ni njia kuu kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za Burundi na Rwanda.

Ameongeza kuwa Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendesha mikutano ya kitaalam kuhusu UKIMWI, Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi, Kupokea tamko litakalotolewa na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Uzinduzi wa taarifa ya tathmini ya Sheria zinazotumika  zinazohitaji kurekebishwa zinazozuia malengo ya sifuri 3.

 Aidha Tume itapokea taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU duniani itakayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuhusu dunia na mapambano dhidi ya VVU.

Dkt. Fatma amefafanua kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine atazindua Mfuko wa UKIMWI ambao utakuwa chachu ya kupunguza maambukizi ya VVU nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia 5.3 huku mikoa ya nyanda za juu kusini ya Njombe, Iringa  na Mbeya ikiongoza kwa kuwa na maambukizi zaidi  na mikoa ya Manyara, Tanga na Lindi  ikiwa na maambukizi ya chini ya asilimia mbili.

Dkt. Kamwela amesema kuwa maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka 19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono yakiendelea kuwa katika hatari ya kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU.

Sababu za uharibifu wa vivuko zatajwa‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +25765056399. 
Na Jovina Bujulu

Uchafuzi wa mazingira katika vituo vya vivuko , utegaji wa nyavu katika njia za vivuko na kukauka kwa maji na kujaa mchanga kwenye njia za vivuko ni sababu zinazochangia kuharibika kwa vivuko nchini.

Hayo yamesemwa leo  jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Ukodishaji mitambo na Huduma za Vivuko kutoka  wakala wa Ufundi wa umeme Tanzania Mhandisi Japhet Maselle.

Aidha, alitaja   sababu za uharibifu wa vivuko hivyo kuwa ni pamoja na baadhi ya abiria kutofuata taratibu za vivuko na wananchi kutumia mitumbwi ambayo si salama kuvukia hasa maeneo ya magogoni Dar es salaam na  Pangani Tanga .

“Utegaji wa nyavu husababisha kunasa kwenye mifumo ya kuendeshea vivuko, na takataka kuingia kwenye mitambo ya kuendeshea vivuko ambapo  husababisha athari katika mitambo hiyo” alisema ndugu Maselle.

Katika kukabiliana na matatizo hayo, TAMESA imeendelea kutoa elimu kwa watu wanaochafua mazingira na maeneo ya vivuko kutangaza taratibu za vivuko ndani ya vivuko  na kuboresha huduma za  vivuko na kuongeza maeneo yenye uhitaji.

Wakala wa ufundi na Umeme Tanzania (TAMESA) ilianzishwa kwa sheria ya wakala namba 30 ya mwaka 1997 ikiwa na lengo la kutoa huduma katika Nyanja za uhandisi mitambo, umeme na uendeshaji wa vivuko .
 
Kwa sasa kuna vivuko 28 vinavyofanya kazi katika vituo 19 Nchini, baadhi ya vivuko hivyo ni Mv Msungwi,Mv sabasaba, Mv Sengerema,Mv mwanza, Mv ukara , Mv Nyerere na Mv Temesa.

Mafundi wazishugulikia mashine za MRI na CT-SCAN Muhimbili.‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mafundi kutoka kampuni ya Philips wanaendelea na matengenezo ya mashine za MRI na CT-SCAN katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zilizopata hitilafu za kiufundi hivi karibuni.

Akizungumza ofisini kwake leo hii Mkuu wa Idara ya Uhusiano Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Buberwa Aligaesha amesema mafundi wapo katika eneo la kazi wakitengeneza hizo mashine ili ziweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Tumepewa siku tatu kukamilisha ukarabati wa hizi mashine hivyo wananchi wawe na subira kwani mashine zikiwa tayari kwa matumizi tutatoa  taarifa” alisema Aligaesha.

Ameongeza kuwa wananchi wawape muda waweze kuzitengeneza mashine hizo ili ziweze kutengemaa kwa ajili ya kutoa huduma za MRI na CT-SCAN hospitalini hapo.

Mashine za MRI na CT-SCAN zilianza kufanya kazi  mara baada ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kutembelea hospitali hiyo hivi karibuni na kuagiza kutengenezwa kwa mashine hizo na baadae kufanya kazi kwa muda wa siku kadhaa na kuharibika tena kutoka na hitilafu za kiufundi.

Wakati alipotembelea Hospital ya Taifa ya Muhimbili jana Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliagiza mashine hizo kutengenezwa,  ndani ya siku tatu  ziwe zimekamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imekuwa ni kimbilio la wananchi wengi kupata huduma za afya hivyo serikali inapamabana kwa kila hali kuhakikisha huduma za MRI na CT-SCAN zinarudi katika hali yake ya kawaida hospitalini hapo.


CHAVITA YASIKITISHWA NA USHIRIKI MDOGO WA VIZIWI KATIKA UCHAGUZI MKUU‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Zawadi Msalla

Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA)   kimeeleza masikitiko yao juu ya ushiriki mbovu wa Viziwi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba  kote nchini.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Habari-MAELEZO leo Mshauri Mwelekezi wa Elimu ya Uraia kwa Watu wenye Ulemavu Bw. Novat Rukwago amesema kuwa, licha ya jitihada mbalimbali ambazo walijaribu kuzifanya ili kuhakikisha viziwi kote nchini wanapata haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupiga kura bado ushiriki wao haukuridhisha.

Rukwago alizitaja changamoto mbalimbali zilizo jitokeza katika uchaguzi  huo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wataalamu wa lugha za alama zinazotumiwa na viziwi katika kampeni mbalimbali za Vyama vya Siasa, hivyo sera na Ilani za vyama hivyo hazikuweza kujulikana kwa viziwi.
“Vyama vingi vilisema ni suala la rasilimali na ukosefu wa fedha za kuweka wataalamu hao, ingawa tuonavyo sisi ni kwamba walishindwa kutoa kipaumbele na si suala la fedha,” alisema Rukwago.

Aidha, Rukwago alisema CHAVITA kwa juhudi binafsi waliweza kutembea jumla ya mikoa 17 kote nchini na kufanikiwa kutoa elimu kwa baadhi ya viziwi ambapo jumla ya viziwi 2516 walijiandikisha, idadi hiyo ikiwa na wanaume 1256 na wanawake 1260. Waliopiga kura walikuwa ni 1807.

Aliongeza kwa kusema kuwa licha ya changamoto hizo pia mazingira ya kupigia kura hayakuwa rafiki kwa watu wenye uhitaji maalumu kwani hakukuwa na wataalamu wa lugha za alama  katika vituo vya kupigia kura.

Waliiomba Serikali kuzingatia umuhimu wa kuyapa kipaumbele makundi mbalimbali yenye uhitaji kwa chaguzi zijazo na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya mawasiliano na vyama vya watu wenye uhitaji maalum mapema ili kuweza kushirikiana katika kuondoa changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu.

WENGI WAJITOKEZA KATIKA UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE JIJINI DAR ES SALAAM

Maelfu wajitokeza katika maandamano ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, hapa wakiendelea na matembezi ya kupinga ukatili wa Kijinsia
  Maandamano yakipokelewa na Mkurugenzi wa shirika la misaada la Marekani USAID  Daniel Moore, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Maire Matthews, Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa Wanawake Lucy Melele, Mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika - WiLDAF, Dr. Judith Odunga, pamoja na wawakilishi wa mashirika wahisani na viongozi mbalimbali.
 Dr. Judith Odunga kutoka WiLDAF akiwakaribisha wageni.
 Mwanaharakati mama Siwale, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mghwira(wa kwanza kulia) ni miongoni mwa waliohudhuria maadhimisho hayo.
 Wageni mbalimbali
 Maigizo kuhusu uchapaji wa viboko kwa wanafunzi
 Mwakilishi wa Balozi wa Ireland Maire Matthews akizungumza
  Lucy Melele kutoka shirika la UN Women akizungumza
 Mwalimu akitoa ushuhuda
  Paulina Mkonongo(wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Akisikiliza jambo
 Mgeni rasmi Bi. Paulina Mkonongo Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi akitembelea sehemu za maonyesho kutoka kwa mashirika mbalimbali.
 Baadhi ya wadau wakitembelea mabanda
 Wadau mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake.

Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake leo yamefunguliwa rasmi kwa kuanza na maandamano ya amani yaliyoanzia uwanja wa Tipi Sinza darajani hadi ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl iliyopo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.

Maandamano hayo yalihudhuriwa na maelfu ya watu yaliongozwa na bendi ya jeshi la polisi kupitia njia za Shekilango kisha barabara ya Morogoro hadi katika jengo la Ubungo Plaza ambapo yalipokelewa na Mkurugenzi wa shirika la misaada la Marekani USAID  Daniel Moore, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Maire Matthews, Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa Wanawake Lucy Melele, Mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika - WiLDAF, Dr. Judith Odunga, pamoja na wawakilishi wa mashirika wahisani na viongozi mbalimbali.

Akitoa neno la ukaribisho, Dr. Judith Odunga alisema kampeni ya siku 16 kwa mwaka huu imelenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni. Lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu mashuleni.

“Ni kutokana na unyeti wa tatizo la ukatili wa kijinsia mashuleni, WILDAF na wadau mbalimbali tumeona kuna umuhimu wa kushirikisha Wizara ya elimu na ufundi stadi ili kuzungumzia ukatili wa kijinsia mashuleni na kujenga mikakati ya kuzuia ukatili huo” Aliongezea.

Dr. Odunga aliitaja kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni FUNGUKA! CHUKUA HATUA, MLINDE MTOTO APATE ELIMU. “Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba shule ni mahala salama. Ni vyema kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu.” Alisema Dr. Odunga.

Dr. Odunga alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kufanya yafuatayo:

1.      Kufutwa kabisa kwa adhabu ya viboko mashuleni na waalimu kufundishwa au kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2.      Kutengeneza mwongozo wa utekelezaji wa sera ya elimu ya mwaka 2014 utakaoelekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3.      Kuboresha miundombinu rafiki ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, madawati, vyoo na sehemu za kujisitiri watoto wa kike, mabweni, uzio pamoja na kuwa na usafiri wa uhakika kwa wanafunzi.
4.      Serikali kuweza kuunda na kusimamia mabaraza yatakayo kuwa yanasikiliza malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5.      Tunaomba Wizara ya elimu na ufundi stadi kushirikiana na wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutunga Sheria ya Ukatili wa Majumbani sambamba na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu ndoa kwa mtoto chini ya miaka 18.


Akifungua rasmi kampeni hizi, mgeni rasmi Paulina Mkonongo ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya sekondari kutoka Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi aliyemuwakilisha Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema, “ukatili wa kijinsia huleta athari hasi katika utoaji na upatikana wa fursa mbalimbali za kijamii ikiwemo fursa ya elimu kwa watoto wetu, hivyo kuwa ni kikwazo katika kujenga usawa wa kijinsia nchini.

Aidha Mkonongo alisema serikali imefanya juhudi za makusudi kuzuia ukatili na kuleta usawa katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kuweka sera na mipango inayozingatia usawa na kupinga ukatili kwa makundi mbalimbali, katika jamii ukiwemo ukatili wa kijinsia.

Mkonongo alitoa wito kwa wananchi wote kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na kwamba kila mtoto ana haki ya kulindwa popote anapokuwepo iwe nyumbani, shuleni, kwenye vyombo vya usafiri, michezoni na njiani wanapokwenda na kurudi shuleni pia kuwapa mbinu za kujilinda wenyewe.

Naye mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Bi. Maire Matthews alisema kuwa takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wastani wa asilimia 45 ya wanawake Tanzania wenye umri kati ya miaka 15 – 49 waliripoti kuwahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono katika maisha yao. Alisema takwimu nyingine zinakadiria kiwango hicho kuwa kati ya 41 – 56%.

Kwa upande wake Lucy Melele kutoka shirika la UN Women aliyemwakilisha Mwakilishi wa shirika hilo hapa nchini Anna Collins alisema wanawake na wasichana ulimwenguni kote wanapitia aina mbalimbali za ukatili ambayo inawanyima haki zao za msingi, ni tishio la demokrasia na ni kizuizi cha amani ya kudumu. Hata hivyo alisema shirika la umoja wa mataifa litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wa maendeleo, serikali, mashirika mbalimbali, na jamii katika kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia pia inafanyika kikanda katika kanda ya ziwa (Mwanza, Mara na Shinyanga, kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga), kanda ya kati (Dodoma, Morogoro na Singida), kanda ya Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa na Lindi, Kanda ya Pwani (Dar es salaam na Pwani) zikisimamiwa na wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya Kivulini, CWCA, NAFGEM, Morogoro Paralegal,  Mtwara paralegal, WiLDAF, TWCWC pamoja na jeshi la Polisi.
WANAHARAKATI WA TANZANIA WANATOA WITO KWA JAMII KUCHUKUA HATUA ILI KUMLINDA MTOTO APATE ELIMU BORA NA SALAMA

  Eda Malick kutoka Tanzania Women and Children Welfare center akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
 Afande Christina Onyango, Afisa wa Polisi, mkoa wa kipolisi Ilala akielezea namna ambavyo dawati la jinsia wamejipanga kufikisha ujumbe wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
  Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini Tanzania wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 Bahati Mandago kutoka shirika la Tanzania Human Rights fountain akielezea mikakati ya shirika lake katika kufikisha ujumbe wa Funguka. Chukua Hatua Mlinde Mtoto apate elimu.

Wadau kutoka katika mashirika mbalimbali wanaoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari
 Dr. Judith Odunga Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF akisoma taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU

Katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia tarehe 25 Novemba mpaka 10 Desemba, WiLDAF, Mashirika ya Haki za Binadamu, Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia watatoa elimu na kuhamasisha umma kuchukua hatua kumlinda mtoto ili apate elimu bora na salama. Ulinzi wa mtoto ni pamoja na kuzuia vitendo vyote  vya ukatili wa kijinsia.

Maadhismisho ya SIku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia mwaka huu yanalenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama  mashuleni, lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu mashuleni, kwani vitendo vingi vya ukatili wa kijinsa vimekuwa vikiripotiwa.

Utafiti uliyofanywa na Chuo cha Tiba Cha Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika, (WiLDAF) umetambua hatari zinazochangia ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na wazazi kutowajali watoto na kutoa adhabu kali kwao na hivyo kuwafanya watoto kuwa na hofu. Wakati mwingine watoto kufanyiwa ukatili bila wao kufahamu. Aidha, adhabu ya viboko inahusishwa kama moja ya aina za ukatili dhidi ya watoto. Hii inaathiri maendeleo ya elimu ya watoto katika taifa letu.

Kukosekana kwa usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike hunapelekea kuwajengea hofu watoto wa kike,  na wakati huo kuwajengea watoto wa kiume ujasiri wa kuona kuwa ni sahihi kwao kufanya  vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Aidha, tafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto (VAC) uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wa mwaka 2011 ulionesha kwamba watoto 3 wa kike kati ya 10 na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume wenye umri kati ya miaka 13-24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, asilimia 6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya tendo la ngono kabla ya miaka 18. Pia utafiti huo unaonesha kuwa watoto wa kike wanafanyiwa vitendo vya kingono  na wanaume waliowazidi umri wakati watoto wa kiume wanafanyiwa ukatili na watoto wenye umri sawa.

Tafiti pia imeonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu wanaowafahamu wakiwemo majirani, wapenzi wao, watu wenye mamlaka (walimu). Ni  asilimia 32.2 tu ya watoto wa kike na asilimia 16.6 ya watoto wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na watu wasiofahamika na watoto. Vitendo hivi hufanyika maeneo ambayo uangalizi wa watu wazima unahitajika kuwepo kwa mfano mashuleni, njiani, majumbani na wakati mwingine katika vyombo vya usafiri.

Ni dhahiri kwamba kwa mazingira, mila na utamaduni ikijumuisha familia za Kitanzania, vimekuwa vikichangia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Vitendo vya ukatili na udhalilishaji vina madhara makubwa ya kiafya kwa watoto kwani hukatisha uwezo wao wa kielimu, mahudhurio ya shule na hivyo kupelekea matokeo mabaya ya  katika ufaulu wao wakati wa mitihani.

Aidha, mazingira yasiyo salama kwa watoto wa shule yana madhara makubwa. Watoto wanapokuwa mashuleni na kufanyiwa ukatili wa kingono wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI kwa mathlani mara tatu zaidi ya wale ambao hawajawahi kufanyiwa ukatili.

Tunaamini kwamba kuondolewa kwa vikwazo vinavyo chochea ukatili wa kijinsia kwa watoto wa shule kutachangia katika kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto wa kiume na wa kike. Pia mazingira mazuri ya shule yatasaidia mahudhurio mazuri ya watoto mashuleni na  kuleta matokeo mazuri katika ufaulu.

Jamii inahaswa kuweka mazingira mazuri ya shule ikiwa ni pamoja na kuwepo miundombinu kama mabweni, vyoo, madawati, uzio kuzunguka mashule na vyombo rafiki vya usafiri. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kutakuwa na dhamira ya dhati kwa watunga sera, wazazi, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla katika kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kuna haja ya makusudi kabisakutofumbia macho  masuala ya ukatili kwa ujumla wake ili kujenga jamii imara.

Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia  ni tukio la kimataifa la kila mwaka ili kuwa na nguvu ya pamoja  katika kuzuia kuenea kwa janga hili . Ndani ya siku hizi, kuna siku zingine muhimu za kimataifa , mathlani, Novemba 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake, Novemba 29 ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni Siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 3 ni Siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu, Desemba 6 ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya kikatili ya Montreal 1989, ambapo wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake. Tarehe hizi zilichaguliwa mahususi ili kuhusianisha kwamba ukatili wa kijinsia unaongeza maambukizi ya UKIMWI na ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.

Katika kipindi hiki cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia , mamia ya asasi za kiraia na wadau mbalimbali Tanzania wataifikia jamii kwa kauli mbiu inayosema;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.

Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya  ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba shule ni mahala salama. Ni vema kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu. Hivyo na haja ya kuwa na taifa linalopiga vita vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Taifa linalofumbia macho ukatili wa kijinsia  haliwezi kupiga hatua kimaendeleo.

Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia ina lengo la kushawishi watunga sera, wadau na jamii kwa ujumla, kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia . Pia ina taka jamii kufichua vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ili kuwa  na jamii isiyovumilia ukatili wa aina yoyote.

Hivyo basi WiLDAF na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaitaka serikali kufanya yafuatayo;
1)    Kufutwa kwa adhabu ya viboko mashuleni na walimu kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2)    Kutengeneza muongozo wa utekelezaji wa sera  ya elimu ya mwaka 2014 utakaolekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3)    Kuboresha miundo mbinu rafiki kwa watoto wa shule ikiwa ni pamoja na  kuwepo kwa vyoo bora, mabweni, madawati, usafiri, uzio kuzunguka shule na mengineyo kwa ustawi wa watoto wa shule.
4)    Kuunda mabaraza yatakayokuwa yanasimamia malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5)    Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya sheria na Katiba zitunge sheria ya kudhibiti Ukatili Majumbani na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971inayoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa, ama kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au Mahakama.

Katika kipindi hiki cha siku 16, za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na shughuli mbalimbali na midahalo ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Tunatoa wito kwa jamii kwa ujumla kupaza sauti na kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Jamii ihamasishe usawa wa kijinsia, mahusiano yasiyo na ukatili na  isibague au kunyanyapaa waathirika wa ukatili wa kijinsia. Tusikae kimya bali tufichue ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua kuwalinda watoto wetu iliwapate elimu bora na iliyo salama. Kwa pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka tunasisitiza;
FUNGUKA!  CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.

Imefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID Tanzania)
Imetolewa na;
Dkt. Judith N. Odunga (MKURUGENZI)
Kwa niaba ya:
Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF)
S.L.P 76215
DAR ES SALAAM    
 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa