Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga
mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Arthur
Mwakapugi tayari kwa ajili ya kusafirishwa leo kwenda kuzikwa kijijini
kwake Ilundo, Wilaya ya Tukuyu mkoani Mbeya.
Mwakapugi, ambaye alifariki dunia akiwa na miaka
64, alitumikia taifa kwa miaka 30 mfululizo kabla ya kufikwa na mauti
Ijumaa saa 3:45 usiku katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete ambaye aliwasili msibani majira ya
saa 11 jioni, nyumbani kwa marehemu Mikocheni B, alitia saini katika
daftari la wageni kabla ya kutoa heshima za mwisho.
Wengine waliotoa heshima zao ni pamoja na Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu Kiongozi
Ombeni Sefue, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Eliakim Maswi na
aliyekuwa Katibu Mkuu, David Jairo pamoja na manaibu makatibu wakuu
wengine kutoka wizara mbalimbali.
Msemaji wa familia ambaye pia ni mjomba wa
marehemu, Mathias Mwambona alisema pamoja na marehemu kustaafu kazi kwa
muda mrefu, serikali kupitia wizara ya nishati na madini imeonyesha moyo
wa kujali, kuthamini mchango wake kutokana na mwitikio waliouonyesha.
“Tunaishukuru sana Serikali pamoja na viongozi,
jamaa na marafiki kwa ujumla, upendo uliojionyesha hauwezi kupimwa kwa
kipimo chochote, wizara na mfanyakazi mmoja mmoja ndiyo wamekuwa mchango
mkubwa katika hatua zote za msiba, kama familia tunawashukuru sana,”
alisema.
Mwakapugi aliyeacha mjane na watoto wawili,
alitumikia nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo Shirika la Viwango
nchini (NBS), Mkurugenzi wa Tume ya Mipango 1999 mpaka 2006 kabla ya
kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini tangu mwaka
2006 mpaka 2010.
Baada ya kustaafu mwaka 2010, Mwakapugu aliendelea
kufanya kazi katika taasisi nyingine zinazojihusisha na masuala ya
kiuchumi kupitia Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini (Repoa).
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
1 comments:
ni wilaya ya rungwe sio tukuyu
Post a Comment