Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » KINANA AWAVAA MAWAZIRI

KINANA AWAVAA MAWAZIRI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Ni Chiza wa Kilimo na Dk.Seif wa Afya
  Wamemkwamisha Rais Kikwete
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana
 
Imetokea tena. Safari hii Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amerejea walichofanya mwaka jana Novemba kwa kutaja mawaziri ambao wameshindwa kutekeleza wajibu wao kuwa ni mizigo, kwa kuwataja mawaziri wawili kuwa wameshindwa kazi na anaomba Rais Jakaya Kikwete awandoe kwa kuwa wamekuwa kiwazo kwake.
Kinana aliwataja mawaziri hao kuwa ni Christopher Chiza wa Wizara hizo ni Kilimo, Chakula na Ushirika na Dk. Seif Rashid wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Alisema wizara zao zimeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi na kwamba watendaji na viongozi hao ndiyo wanaomwangusha Rais Kikwete.

Kinana alisema kwamba Rais Kikwete anakwamishwa na watendaji wachache aliowaweka serikalini na kueleza wazi kuwa wizara hizo zinazokwamisha juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kinana alisema Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inamuangusha Rais Kikwete kwa kutowajali wakulima na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa vituo ya afya na zahanati pamoja na kutosajili zahanati mpya.

Kinana aliitoa kauli hiyo wilayani Tabora katika mkutano wa hadhara juzi jioni wa majumuisho ya ziara yake ya siku 11 katika mkoa wa Tabora kabla ya kuanza ziara ya mikoa ya Singida na Manyara jana.

Akihutubia mamia ya wananchi, alisema anashangazwa na wizara husika kusikia malalamiko ya wananchi na kukaa kimya, hali inayowafanya wananchi kukosa msaada na kubaki wakiumia wakati watendaji wakiwa maofini wakisubiri mishahara.

Alisema Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika inalalamikiwa na wakulima wa tumbaku wa mkoa huo, lakini imeendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote, hali inayowafanya wananchi waichukie serikali.

“Rais Kikwete anakwamishwa na baadhi ya watendaji ambao amewapa dhamana ya kusimamia sekta mbalimbali, haiwezekani tangu nimeanza ziara katika mkoa huu, vyombo vya habari vinaripoti matatizo ya wakulima wa tumbaku, lakini Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza na watendaji wake wameendelea kuwa kimya tu hadi leo, kama hawasikii kinachoendelea vile,” alisema Kinana.

Alisema matatizo yaliyoko katika wizara hiyo ni makubwa hasa kwa wakulima wa tumbaku, kwani hadi sasa wanadai fedha za tumbaku walizokopesha vyama vya ushirika Sh. bilioni 28, ambazo hakuna katibu wa wizara wala mtendaji ambaye amezizungumzia au kutafuta suluhisho.

“Matatizo ya wakulima nimeyasikia na tutakwenda kushikana mashati kwenye vikao vyetu na hawa wakubwa, nina imani Rais Kikwete atachukua hatua dhidi yao, haiwezekani watendaji wachache wanaojifanya miungu watu wakachafua sifa ya chama na serikali, kwa kushindwa kusimamia miradi waliyopewa, bado wakaendelea kuwapo,” alisema Kinana.

Kuhusu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kinana alisema imeshindwa kusimamia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya wakati mpango wa serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati.

Kinana alifafanua kuwa wizara hiyo imempa kazi mkandarasi ambaye ameshindwa kuifanya na kusababisha miradi ya ukarabati wa zahanati na vituo vya afya kukwama na wananchi wakiendelea kuumia huku watendaji wakiwa kimya.

“Mfano hospitali ya Kitete nimeshuhudia majengo hayajakarabatiwa kwa miaka mitatu sasa tangu mkandarasi amepewa fedha ya kufanya kazi hiyo… watendaji, makatibu na wizara nzima wako wapi kusimamia haya, na kwa nini wasimchukulie hatua huyu aliyeshindwa kukamilisha kazi hii,” alihoji Kinana.

Alisema katika wilaya za Nzega na Igunga wananchi wamejitolea kujenga zahanati 70, lakini watendaji na viongozi wa wizara wameshindwa kuzipa usajili, hali inayowafanya wananchi hao washindwe kuendelea na kazi nyingine za miradi kutokana na kukosa ufuatiliaji wa karibu wa viongozi.

Alisema ni vyema viongozi na watendaji wa serikali wanaokwamisha miradi wakachukuliwa hatua stahiki ili kutoa fundisho kwa watendaji wengine.

 “Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ukitaka kusafisha nyumba itakate ni vyema ukafagia na Shilingi ili kutoa taka zote, kwa maana kwamba viongozi msiogope kuwafukuza wanaokwamisha maendeleo kwa kuogopa kuwafukuza wasiohusika, ukifukuza utendaji utakuwapo kwa watumishi,” alisema Kinana.

Kauli za Kinana ni mwendelezo wa CCM kuwatuhumu baadhi ya mawaziri kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

Novemba mwaka jana akiwa katika ziara ya mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma, Kinana na Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, waliwatuhumu baadhi ya mawaziri kwamba wameshindwa katika utendaji wao na kukwamisha utekeleza ilani ya CCM na kuapa kwamba wataitwa kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ili baadaye wawajibishwe na Rais Kikwete.

Mawaziri waliotuhumiwa ni Chiza na aliyekuwa naibu wake, Adam Malima (sasa Naibu Waziri Wizara ya Fedha) kwamba wameshindwa kutatua matatizo ya wakulima wa korosho na mahindi.

Mwingine ni Waziri wa Elimu na mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kwamba wakati akiwa Waziri wa Miundombinu alitoa zabuni ya ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo kwenda Tunduru kwa kampuni ambayo ilishindwa kuijenga.

Hata hivyo, licha ya kuhojiwa na CC, Rais Kikwete hakutengua uteuzi wao.

Jana Waziri Chiza hakupatikana kuzungumzia madai hayo kutokana na kuwa nje ya nchi kikazi.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Godfrey Zambi, alisema kuwa baada ya wizara kupata malalamiko ya wakulima katika maeneo kadhaa ya nchi, iliiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi na baada ya kuandaa taarifa, wizara itaitumia kufanya maamuzi.

Hata hivyo, Dk. Rashid na Naibu wake, Kebwe Stephen Kebwe, jana hawakupatikana. Wote simu zao zilikuwa zinaita bila majibu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa