Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Profesa Sospeter Muhongo
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, wizara hiyo itawasilisha makadirio yake ya bajeti kwa mwaka 2014/15 Mei 29, mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, DK. Edward Hoseah, akizungumza katika mahojiano na NIPASHE jana, alisema taasisi hiyo imeanza kuchunguza madai hayo na kwamba kwa hatua ya kwanza ataitwa Waziri Muhongo kuhojiwa.
“Tunalishughulikia, lakini hatuwezi kulipa kipaumbele sana, nimemwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma amwite Waziri Muhongo amhoji kuhusiana na taarifa hizi za kuhongwa wabunge na baada ya hapo watahojiwa watu wengine,” alisema Dk. Hoseah.
Dk. Hosea alisema taasisi hiyo imeamua kumwita na kumhoji Prof. Muhongo kutokana na kulalamika bila kutoa taarifa za tuhuma hizo kwa Takukuru.
Wakati Takukuru ikifanya mchakato wa kumhoji waziri huyo, taarifa za ndani kutoka Wizara ya Nishati na Madini zinaeleza kuwa kutokana na sakata hilo bajeti ya wizara ilipangwa kuwasilishwa bungeni wiki hii, lakini imesogezwa hadi Mei 29.
Kuna mvutano kati ya Waziri Muhongo na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, ambao unadaiwa kusababishwa na ujumbe wa maandishi wa kutaka kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kusambazwa kwa baadhi ya wabunge.
Ujumbe huo mfupi unamtuhumu Mkono kula njama za kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambao unadaiwa kutumwa na Waziri Muhongo kwenda kwa baadhi ya wabunge akimtuhumu Mkono kuwahonga baadhi ya wabunge Sh. milioni tatu kila mmoja ili kukwamisha bajeti hiyo.
Ujumbe huo unasomeka: ”Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Sisi wabunge waadilifu tunakiri kwamba Mheshimiwa Mkono ametufuata na kutupatia fedha kila mmoja Shilingi milioni tatu ili tukwamishe bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.”
MAJIBU YA MUHONGO
Alipoulizwa Prof. Muhongo kuhusiana na mvutano kati yake na Mkono, alisema: “Mimi sijamtuhumu, subirini wakati ukifika mtaujua ukweli.”
“Mengi yanasemwa, lakini siku nikizungumza ukweli utajulikana, mimi siyo Mswahili na siwezi kujibishana kupitia kwenye magazeti,” alisema alipozungumza na NIPASHE jana jioni.
Alipouliza kuhusu kuhojiwa na Takukuru, alisema: “Wewe umesema Takukuru wamenihoji, nenda ukawaulize kama wamenihoji halafu ukae uandike, uchekelee, dunia nzima ijue.”
Hii ni mara ya pili Profesa Muhongo anaingia kwenye malalamiko ya kutuhumu wabunge kupokea rushwa ili kukwamisha bajeti ya wizara yake.
Mwaka juzi wakati wa mkutano wa bunge kama huu aliwatuhumu baadhi ya wabunge kuwa wamehongwa na kampuni za mafuta ili kukwamisha bajeti yake, hali ilimfanya Spika wa Bunge Anne Makinda kuunda kamati teule iliyoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Kamati hiyo pia ilichunguza tuhuma za ufisadi wa wabunge kuhusika na ufisadi wa Tanesco. Hata hivyo, baada ya uchunguzi mrefu tuhuma za Muhongo dhidi ya wabunge hazikuthibitika.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment