Home » » DALADL ZAGOMA DAR

DALADL ZAGOMA DAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga
 
Abiria wanaotoka Ubungo kwenda  Tegeta kupitia Mwenge jijini Dar es Salaam jana walilazimika kutembea kwa mguu, baada ya madereva wa daladala zinazofanya safari katika maeneo hayo kugoma wakidai kuonewa na askari wa usalama barabarani.
Madereva hao walidai kuwa wamekuwa wakikamatwa na askari bila sababu na kupigwa faini kubwa kwa makosa ambayo hayawezi kuepukika kutokana na mamlaka husika kuchangia makosa hayo.

Wakizungumza na NIPASHE, madereva hao walisema askari wa usalama barabarani wanawalazimisha washushe na kupakia abiria kituo cha Mawasiliano Tower na kurudi Mwenge, agizo ambalo ni gumu kutekelezeka kutokana na mazingira yalivyo.

Alli Yusuf, Katibu wa madereva hao alisema walitukataza kwenda kushusha katika kituo cha daladala eneo la Tanesco kutokana na ujenzi wa barabara ya mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART).

“Tunaweza kujibana hapa darajani, lakini wakikuona tunashusha wanakufuata na kukuandikia faini ya kuanzia Shilingi 90000 mpaka 100,000, kiwango ambacho ni kikubwa mno,” alisema Yusuf.

Yusuf alisema wamekuwa wakipewa risiti ambazo zinaonekana ni feki kutokana na kuandikwa mwaka 2011 na nyingine mwaka 2010 badala ya mwaka 2014 na wakihoji wanaambiwa hawana haki.

“Ukiangalia risiti hizi zimeandikwa miaka ya nyuma wakati kila mwaka serikali inafanya hesabu, kwa hiyo hizi fedha hazifiki ofisini na hawa jamaa wanasema wameagizwa na bosi wao kuwa wahakikishe wanafikia malengo ambayo sisi hatuyajui,” alisema.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Mohamed Mpinga, alisema suala la kukamatwa kwa daladala ni la kawaida kwa kuwa wanapovunja sheria ni lazima waadhibiwe.  Kuhusu jeshi hilo kutoa risiti za miaka ya nyuma, alisema bado hajapokea taarifa, lakini atalishughulikia.

“Sijapokea taarifa kama hiyo ila kwa kuwa umeniambia, nitaifanyia kazi kwani risiti zetu huwa haziandikwi mwaka wala tarehe, halafu kama kuna malalamiko ni muhimu wakapeleka kwa RTO (Mkuu wa Trafiki Mkoa) husika kuliko kukimbilia kugoma na kusababisha adha kwa abiria,” alisema Mpinga.

Mkurugenzi wa wa Manispaa ya Kinondoni, Musa Natti, alisema: “Mimi najua kituo cha daladala cha Ubungo bado hakijakamilika na anayetoa taarifa ni sisi halmashauri kwani ilishindikana kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha, lakini baada ya mvua kukatika, kitakamilia.”

Hata hivyo,  msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), David Mziray, jana hakupatikana kutokana na simu zake zote za kiganjani kutopatikana.

Baadhi ya abiria waliiomba serikali iingilie kati suala hilo kwa kuwa wanapata shida kutembea kwa miguu kutoka Ubungo mpaka Mwenge.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa