Home » » WANASIASA WAELIMISHWA KUTUMIA KAMPENI ZA 2015 KUELEZEA UKIMWI

WANASIASA WAELIMISHWA KUTUMIA KAMPENI ZA 2015 KUELEZEA UKIMWI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
 
Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kutumia majukwaa kwa ajili ya kuelimisha wananchi juu ya ugonjwa wa Ukimwi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Frolence Turuka, katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wakati wa   ufunguzi wa semina ya mapambano dhidi ya Ukimwi iliyoandaliwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama kwa wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa.

“Mwaka 2015 ni mwaka wa uchaguzi mkuu,  huu ni wakati ambao vyama vya siasa vinakuwa kwenye mchakato wa kumpata kiongozi mkuu wa nchi yaani Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani  na vile vile,  hii ni fursa nzuri kwa wagombea kunadi sera za vyama bila kusahau tatizo la Ukimwi,” alisema Dk. Turuka.

Alisema wagombea wanatakiwa kujua maradhi yanayowapata wananchi ukiwamo Ukimwi.

Alisema ufahamu huo utawasaidia katika kutunga sera, sheria na kanuni mbalimbali katika kukabiliana na changamoto zitokanazo na madhara hayo wapatapo ridhaa ya wananchi kuwa viongozi wao.

“Naamini kupitia semina hii mtaziangalia kwa kina ilani zenu na kuboresha ili ziweze kubeba ajenda ya Ukimwi, mtaainisha maeneo ya kufanyia kazi na namna ya kushirikiana na Tacaids pamoja na wadau wengine katika kupiga vita dhidi ya ugonjwa huu,” alisema.

Alisema Ukimwi ni janga la Kitaifa na hauchagui chama, kabila, dini, uraia, rika, ukanda wala elimu.

Kaimu Mwenyekiti Mtendaji wa Tacaids, Jumanne Isango, aliyezungumza kwa niaba ya  Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, Dk. Fatma Mrisho, alisema harakati hizo zitatoa fursa kwa viongozi wa kisiasa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa