Home » » KAMATI YA NIDHAMU TFF YATOA UAMUZI RUFANI YA YANGA

KAMATI YA NIDHAMU TFF YATOA UAMUZI RUFANI YA YANGA


Kamati
ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesikitishwa
na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo
namba 132 wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yao na Azam uliofanyika
Machi 10 mwaka huu.
Vilevile imesikitishwa na uongozi wa klabu ya Yanga kushindwa kuvikemea hadharani vitendo hivyo vilivyofanywa na wachezaji wake.
Kamati
hiyo ilikutana jana (Aprili 4 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake
Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana kujadili rufani
iliyowasilishwa mbele yake na Yanga kupinga uamuzi uliofanywa na Kamati
ya Ligi ya TFF dhidi ya wachezaji hao.
Mbele
ya Kamati hiyo, Yanga ilikuwa na rufani mbili. Rufani ya kwanza ya
Machi 11 mwaka huu iliomba matokeo ya mchezo huo yafutwe, ikiwemo kadi
walizooneshwa wachezaji wao na mwamuzi aadhibiwe kwa kushindwa kumudu
mchezo huo.
Wakati
ikifanya mawasilisho (submissions) mbele ya Kamati, Yanga iliamua
kuondoa rufani hiyo kwa vile katika ya pili iliyokatwa Machi 14 mwaka
huu ikipinga adhabu zilizotolewa ina kifungu (j) kilichodai Kamati ya
Ligi ya TFF ilikosea kutotoa uamuzi wowote kwa refa aliyedaiwa kutoa
maneno ya kashfa na kejeli kwa wachezaji wao.
Baada
ya kusikiliza submissions za pande zote mbili (walalamikaji- Yanga)
ambao walikiri hatia ya vitendo hivyo na kuomba wachezaji wake
wapunguziwe adhabu, na (walalamikiwa- TFF), Kamati imetoa uamuzi
ufuatao;
Mchezaji
Nurdin Bakari amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu za ligi na faini
ya sh. milioni moja. Omega Seme amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu
na faini ya sh. milioni moja.
Nadir
Haroub atatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu na faini ya sh. 500,000
kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ambayo haikatiwi rufani. Lakini Kamati ya
Nidhamu imeondoa adhabu ya mechi nyingine tatu iliyotolewa na Kamati ya
Ligi ya TFF kwa vile hizo atazitumikia kwa pamoja, lakini adhabu ya
faini ya sh. 500,000 inabaki, hivyo atalipa jumla ya sh. milioni moja.
Stephano
Mwasika ambaye alifungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja,
adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za msimu wa
ligi 2011/2012, lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili.
Kwa
upande wa Jerryson Tegete aliyefungiwa miezi sita na faini ya sh.
500,000, adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za
ligi msimu huu (2011/2012), lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni
mbili.
Adhabu
ya Yanga kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki
wake inabaki kama ilivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1). Vilevile adhabu
ya faini ya sh. 500,000 kutokana na timu hiyo kupata kadi tano na
kuendelea kwenye mechi moja inabaki kama ilivyo vile kanuni ya 25(1)
haikatiwi rufani.
Kamati
imesema adhabu zimeanza kutumika tangu zilipotolewa na Kamati ya Ligi,
hivyo kwa ambao tayari wameshatumikia mechi kadhaa zinahesabika. Kwa
watakaoshindwa kulipa faini wataendelea kuwa nje ya uwanja mpaka fedha
hizo zitakapolipwa.
Mwenyekiti
Tibaigana amewataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji
wao, na makosa hayo yakijirudia adhabu kali zaidi zitatolewa.
Pia
Kamati ya Nidhamu ya TFF haikujadili suala la Yanga kunyang’anywa
pointi tatu katika mchezo kati yake na Coastal Union kwa vile hakukuwa
na rufani hiyo mbele yake.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa