Home » » MKUTANO MKUU WA 28 WA JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT) KUFANYIKA MEI 3-5 KATIKA HOTELI YA KUNDUCHI BEACH JIJINI DAR ES SALAAM

MKUTANO MKUU WA 28 WA JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT) KUFANYIKA MEI 3-5 KATIKA HOTELI YA KUNDUCHI BEACH JIJINI DAR ES SALAAM


 Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Meya wa Jiji la Dar es
Salaam, Dk. Didas Masaburi (katikati), akizungumza na waandishi wa
habari jijini jana kuhusu Mkutano Mkuu wa 28 ALAT utakaofanyika Mei 3 – 5
mwaka huu katika Hoteli ya Kunduchi Beach.  Kushoto ni Meneja wa Huduma
kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Muungano Saguya na
Katibu Mkuu wa ALAT, Habraham Shamumoyo.
 Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Meya wa Jiji la Dar es
Salaam, Dk. Didas Masaburi (wa pili kushoto),akizungumza na waandishi
wa habari jijini Leo Aprili 24.12, kuhusu Mkutano Mkuu wa 28 ALAT
utakaofanyika Mei 3 – 5 mwaka huu katika Hoteli ya Kunduchi Beach.
Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Kushoto ni Meneja wa Huduma kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC), Muungano Saguya na (wa tatu kushoto), ni Katibu Mkuu wa ALAT,
Habraham Shamumoyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Vision Investments waratibu
wa Mkutano huo, Bw. Ali Nchahaga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vision
Investments waratibu wa Mkutano huo, Bw. Ali Nchahaga (wa pili kushoto),
akiwa kazini na kikosi kazi chake. Kushoto ni Mdau wa ALAT.Picha na John Badi
---
Jumuiya
ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) itakua na Mkutano Mkuu wa 28 tarehe 3
– 5 Mei 2012. Mkutano huo utafanyika hapa Dar es Salaam kwenye hoteli
ya Kunduchi Beach.


Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 28 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) ni “Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi”. 

ALAT
imedhamiria kutumia Mkutano wake Mkuu wa Jumuiya kwa mwaka huu kuwa
jukwaa la kupeana uzoefu wa ushirikiano baina ya sekta ya Umma na Sekta
binafsi (PPP).

Hii inatokana na sheria ya ubia iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania The Public Private Partnership (PPP Act) 2010. 

Mkutano
huo ambao utafanyika tarehe 04- 05 Mei 2012, utatanguliwa na jukwaa la
ubadilishanaji uzoefu juu ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi
katika kutoa huduma kwa jamii na hasa katika kuzitumia Serikali za
Mitaa.


Ifahamike ya kwamba Serikali za mitaa sawa na majukumu yake, ndio zenye
fursa ‘potential’ kubwa  na  nyingi za kutekeleza ubia kwa kufanya
mashirikiano yenye manufaa na sekta binafsi. 

Jumuiya
imeona haja na umuhimu wa kuandaa jukwaa hili kwa wanachama wake kwani
ni lenye manufaa makubwa ya kuwafanya viongozi na watendaji wa
Halmashauri zote nchini kuweza  kujifunza na kufahamu dhana nzima lakini
pia utendekaji halisi (Practicality) wa ubia. 

Hii
pia ni fursa ya pekee kwa sekta binafsi, taasisi za Serikali na
mashirika ya Umma kuweza kushiriki pamoja na viongozi na watendaji wa
Serikali za Mitaa kujadili jambo lenye manufaa kwa pande zote.


Aidha Jumuiya inatoa nafasi chache za udhamini wa Mkutano Mkuu ambao pia
utatoa fursa ya kushiriki moja kwa moja katika jukwaa hilo.


Jukwaa la ubadilishanaji uzoefu litakaloongozwa na mtaalamu aliyebobea
wa kimataifa katika nyanja za ubia baina ya sekta ya umma na binafsi
(PPP), litajadili mada mbalimbali zinazohusu ubia.


Mada hizo ni pamoja na maana halisi ya ubia, je ni ubinafsishaji?; njia
mbalimbali za kufanya ubia; msingi wa kisheria wa ubia, uzoefu wa
halihalisi ya ubia kimataifa; dhati/dhamira hasa ya ubia;  faida
zinazoweza kupatikana kutokana na ubia; Mchakato wa ufanyikaji wa ubia
na Uchaguaji wa miradi na upembuzi yakinifu. Mada nyingine ni Utambuzi
wa viashiria vya hatari (risks) uchambuzi wake na upunguzaji; fursa za
kifedha katika ubia; njia muafaka katika manunuzi; usimamizi wa ubia,
uangalizi na tathmini.   


Mkutano Mkuu wa kawaida wa Jumuiya hufanyika mara moja kila mwaka na
wajumbe wake ni kama ifuatavyo: Wenyeviti na Mameya 133 wa Halmashauri
za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya, Wakurugenzi 133 wa Halmashauri,
Wabunge 21 mmoja toka kila mkoa.

 Mkutano
huu utahudhuriwa pia na Wizara, Idara za Serikali Kuu, Wakala za
Serikali, Taasisi shiriki katika Serikali za Mitaa, wawakilishi wa
Balozi na Wabia katika Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa na Jumuiya za
Serikali za Mitaa za Afrika Mashariki na wadau wangine wa sekta ya
Serikali za Mitaa. 

Aidha
Mkutano huu utahudhuriwa na Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika na
Makampuni na Wawakilishi wa Sekta Binafsi. Inatarajiwa kwamba Mkutano
huu utahudhuriwa na Washiriki takribani mia tano (500).


Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ni chombo kinachoziunganisha
Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji Tanzania Bara. Kwa
sasa kuna Halmashauri 133 zinazounganishwa na chombo hiki.

 
Dira
ya Jumuiya ni kuwa na Serikali za Mitaa zinazojitegemea na zenye
ufanisi katika kutoa huduma zinazokidhi viwango kulingana na vipaumbele
vya wananchi wake.


Mwelekeo wa Jumuiya ni kutambulika kama chombo na sauti ya pamoja ya
Mamlaka za Serikali za Mitaa ikitoa huduma za kitaalamu na kiufundi kwa
wanachama wake.


Katika mkutano huo Jumuiya imemwalika Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgeni rasmi.


Aidha watu mashuhuri wakiwemo viongozi wa Serikali na Sekta binafsi
wamealikwa kutengeneza jopo la wasemaji. Miongoni mwa wanaotarajiwa ni
Mhe. Mustafa Mkulo Waziri wa Fedha, Mhe. William Ngeleja Waziri wa
Nishati na Madini, Mhe. kapteni Mstaafu George Mkuchika Waziri wa
TAMISEMI, Mhe. Gaudensia Kabaka Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Emanuel
Nchimbi Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mhe.  Profesa Ana
Tibaijuka Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mhe. Ezekiel
Maige Waziri wa Maliasili na Utalii.


Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dr.Cyiril Chami, Waziri wa
Mambo ya Ndani Mhe. Shamsi Nahodha, Waziri wa Kilimo na Ushirika Mhe.
Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Mifugo Dr. Mathayo David Mathayo. 

Walioalikwa
wengine ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini Bwana Harry Kitilya, Inspekta
Jenerali wa  Polisi, Saidi Mwema, Bi Esther Mkwizu Mwenyekiti wa Mfuko
wa Sekta Binafsi, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Huduma za Manunuzi Dr.
Ramadhani Mlinga pamoja na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

 
Kwa
namna ya pekee na kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais, Jumuiya
imemwalika Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Fedha za Serikali (CAG)
Ndugu Ludovick Utouh ambaye atawasilisha Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu
za Fedha za Serikali za Mitaa.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa