Home » » Wanaogombea Ubunge Afrika Mashariki Wachujwa

Wanaogombea Ubunge Afrika Mashariki Wachujwa


Fidelis Butahe
JOTO la kuwania nafasi za ubunge wa Afrika Mashariki (EALA), kupitia CCM limezidi kupanda baada ya juzi kukamilika kwa hatua ya pili ya mchujo, iliyowezesha wanachama 24 kusubiri mchuano bungeni kuwania nafasi nane za kukiwakilisha chama hicho.

Katika kinyang'anyiro hicho upinzani una nafasi moja ili kukamilisha idadi ya wabunge tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika bunge hilo la Afrika Mashariki.

Uchaguzi huo uliofanyika Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam chini ya uoenyekiti wa wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ulijaa kila aina ya vituko ikiwa pamoja na mgombea kwa upande wa wanawake Bara, Godbertha Kinyondo kukaukiwa sauti wakati akijinadi na kuomba kura.

Hali hiyo ilimlazimu mgombea huyo kuomba kura kwa ishara akiacha wajumbe kuangua kicheko ukumbini humo. 
Akitangaza matokeo hayo Pinda alisema katika kundi la wanawake kutoka Zanzibar waliopita na kura zao kwenye mabano ni Septuu Nassor (177), Safia Ali Rijaal (169) na Mariam Usi Yahaya (179).

Katika kundi la wanaume upande wa Zanzibar waliopita ni Dk Said Bilal (197), Abdallah Ali Mwinyi(187), Zuber Ali Maulid (176), Dk Haji Mwita Haji (168), Amada Khatibu (167) na Hamis Jabir Makame (143).

Kwa upande wa wanawake Bara waliopita ni Angela Kizigha (160), Janeth Mmari (133), Janet Mbene (116), Fancy Nkuhi (147), Shyrose Bhanji (145) na  Godberha Kinyondo (115).

Wanaume Bara waliopita ni Adam Kimbisa (196), Dk Edmund Mndolwa (159), Siraju Kaboyonga (153), Bernard Mulunya (143), William Malecela (136), Elibariki Kingu (132), Evance Rweikiza (125), Mrisho Gambo (121) na Charles Makongoro Nyerere (113). Chanzo: Mwananchi.
Habari kwa hisani ya Mjengwa blog

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa