Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi aliyeshika kiti akitembelea mabanda ya maonyesho ya wauguzi.Kushoto kwakwe ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Joseph Kuzilwa.
Mh. Waziri pamoja na Mwenyekiti wa Bodi wakisalimiana na Viongozi wa TANNA Muhimbili kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa CPL
Sehemu tu ya Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ndani ya ukumbi wa CPL wakisimama kumkaribisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
Mh. Waziri Dkt Hussein Mwinyi akizungumza na Wauguzi kama wanavyomsikiliza katika picha inayofuata hapo chini
Mwenyekiti wa TANNA Tawi la Muhimbili Bw. Paul Magesa pamoja na Prof. Kuzilwa wakitoa zawadi ya pongezi kwa Mh. Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi kuteuliwa kushika wadhifa huo
====== ===== ======
Siku mbili tu baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mh. Dkt.Hussein Mwinyi kuingia ofisini, amehahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wauguzi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kiutendaji.
Hayo aliyasema leo wakati akizindua Kongamano lililoandaliwa na Chama cha Wauguzi Tanzania Tawi la Muhimbili ambao wataungana na Wauguzi wote duniani kuadhimisha siku ya Wauguzi Duniani inayotarajiwa kufanyika Mei 12, 2012.
Dtk. Mwinyi alisema nafasi ya wauguzi katika sekta ya afya ina umuhimu wa pekee kwani muda mwingi wao ndio wanaokaa na wagonjwa hivyo kazi yao ni kubwa na wanastahili kupongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Aidha alisema ofisi yake itakuwa wazi na inakaribisha majadiliano na wauguzi katika kutafuta ufumbuzi kwa pamoja na mapema wa changamoto zinazowakabili wauguzi badala ya kusubiri mihadhara kama hii kusema changamoto zao.
Aliwashuruku Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa jinsi walivyotoa huduma bila kuchoka katika kipindi cha migomo iliyojitokeza hivi karibuni. Aliwasifu na kuomba jamii itambue mchango wao mkubwa walioutoa katika kuhudumia wagonjwa.
Chama cha Wuguzi Tanzania (TANNA) Tawi la Muhimbili kimeandaa maonyesho ya huduma wanazotoa ambayo yanafanyika ndani ya Hospitali na kutoa huduma za kupima sukari, shinikizo la damu, maambukizi ya UKIMWI, usikivu, ushauri nasaha pamoja na kuhamasisha wananchi kujitolea damu. Maonyesho haya yanaendana sambamba na kongamano la kisayansi la wauguzi linalofanyika ndani ya Hospitali ambapo wadau na wauguzi toka Hospitali za nje ya Jiji la Dar Es Salaam wameshiriki.
Wakati huo huo TANNA Muhimbili imempa zawadi Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Njelekela kwa kutoa ushirikiano wa karibu sana kwa wauguzi katika kipindi cha miezi sita aliyoshika nafasi hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Sr. Agnes Mtawa alisema Mkt. Njelekela ameonyesha upendo na ushirikiano mkubwa kwa wauguzi na kila mara amekuwa akitoa muda wake mwingi kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Picha na Jiachie Blog





0 comments:
Post a Comment