Home » » 540 yawaomba radhi abiria wake

540 yawaomba radhi abiria wake


Na Oliver Oswald, Dar es Salaam
UONGOZI wa Shirika la Ndege la 540, umewaomba radhi abiria wake kwa usumbufu walioupata baada ya moja ya ndege zake kupata hitilafu wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa shirika hilo, Brown Francis, alisema kuwa, wana kila sababu ya kuomba radhi kwa kuwa abiria walipata shida kutokana na hitilafu ya ndege hiyo.

“Tukio hili ni la mara ya kwanza kutokea katika shirika letu na sisi kama uongozi, tulishtushwa na tukio hili kwa kuwa halijawahi kutokea na tunawaahidi abiria wetu wote, kuwa jambo hili halitajirudia.

“Wakati wa tukio hilo, abiria 35 waliokuwa Mwanza na wengine 26 waliokuwa Kilimanjaro wakitaka kuja Dar es Salaam walishindwa kusafiri kutokana na tatizo hilo.

“Kwa hiyo, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba radhi abiria wote kwa usumbufu mkubwa uliojitokeza, kwani ulisababishwa na kukosekana kwa mawasiliano ya moja kwa moja baina ya abiria wetu na uongozi wa shirika.

“Baada ya tatizo kutokea tuliwataarifu abiria wetu na kuwapeleka hotelini kwa kuwaahidi kuwa, tungewafuata asubuhi ya siku inayofuata kwa ajili ya safari yao kwa kuwa tulikuwa na uhakika wa kupata kifaa kilichokuwa kinahitajika kwenye ndege.

“Kwa bahati mbaya, tulishindwa kukipata kifaa hicho kwa muda tuliotarajia, kwa hiyo, tukashindwa kuwafuata abiria hotelini muda tuliowaahidi kwa kuwa ndege ilikuwa bado ina matatizo.

“Kwa kuwa muda wa kuwafuata ulikuwa umepita, abiria waliamua kuondoka hotelini moja kwa moja hadi uwanja wa ndege zilipo ofisi za shirika letu ili kujua hatima ya safari yao.

“Uongozi wa shirika ulipojua kuwa abiria hao wapo maeneo hayo, ulifika na kuwaelewesha kilichotokea na kuwaahidi kuwa ndege hiyo ingewasili na kuondoka siku hiyo na ilipowasili majira ya saa 8 alasiri walisafirishwa,” alisema Francis.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa