Home » » Hospitali ya Regency yafanya upasuaji kwa kutumia kamera

Hospitali ya Regency yafanya upasuaji kwa kutumia kamera


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Regency ya Dar es Salaam imeanzisha programu ya upasuaji wa maradhi mbalimbali ya tumbo kwa njia ya teknolojia ya kisasa ya kutumia kamera.
Upasuaji huo ambao mgonjwa hapasuliwi sehemu kubwa, unahusisha kupasua tundu dogo tumboni na kuingiza kifaa chembamba ambacho huonyesha picha ya tatizo husika katika televisheni na hatimaye daktari kufanya matibabu bila kupasua sehemu kubwa ya tumbo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency, Dk. Rajni Kanabar, utaratibu huo mpya utapunguza gharama kwa wagonjwa kwenda India na nchi mbalimbali kwa ajili ya upasuji wa aina hiyo ambao ndio kwanza umeanzishwa na hospitali hiyo.

“Badala ya kwenda nje ya nchi, kwa ajili ya upasuaji huu wa kisasa, watu watapata fursa ya kufanyiwa upasuaji hapa hapa nchini, hii itaokoa fedha na muda na tangu tuanze huduma hii miezi miwili iliyopita, wagonjwa 35 wameshapasuliwa na wanaendelea vizuri,” alisema Dk. Kanabar.

Daktari bingwa anayefanya upasuaji huo, Rajeev Tandon, alisema kwa upasuaji wa kawaida, daktari hutarajia kufanya upasuaji mkubwa ili kufikia viungo anavyohitaji tumboni, hali inayosababisha maumivu makali kwa mgonjwa na kutopona haraka.

“Upasuaji huu wa kisasa tunaofanya hapa Regency unamfanya daktari kufikia viungo anavyotaka kupitia matundu madogo tumboni, hii inasaidia mgonjwa kubaki bila makovu baada ya kupona, kupona haraka na kuendelea na shughuli zake saa moja tu baada ya upasuaji, tofauti na upasuaji wa kizamani ambapo humchukua muda mrefu mgonjwa kupona,” alisema Dk. Tandon.

Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa aina hiyo Juni 21, mwaka huu, alisema alikuwa akisumbuliwa maumivu makali na kutapika kwa miezi kadhaa, lakini baada ya upasuaji anaendelea vizuri.

Alisema hivi sasa anaendelea na kazi zake za kila siku bila kusumbuliwa na maumivu ya aina yoyote
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa