Na Hellen Ngoromera, Dar es Salaam
TAKWIMU za Shirika la Under the Same Sun (UTSS), zinaonesha kwamba watu 71 wenye ulemavu wa ngozi (albino) wameuawa nchini hadi sasa.
Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Meneja Operesheni wa shirika hilo, Gamariel Mboya, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali wanayofanyiwa albino.
Alisema pamoja na mauaji hayo, albino wengine 28 wamejeruhiwa kutokana na kufanyiwa vitendo vya mashambulizi, na makaburi 18 ya walemavu hao yakifukuliwa.
“Takwimu hizo ndizo tulizokuwa na ushahidi nazo… watu walioshambuliwa kwa namna tofauti ikiwemo kutishiwa na wengine kukatwa sehemu za miili yao, ikiwemo mikono, miguu na nyingine, na wengine kwa makaburi yao kufukuliwa baada ya kufariki na viungo vyao kuchukuliwa,” alisema Mboya.
Pamoja na mambo mengine, UTSS ilielezea kusikitishwa na kufadhaishwa na mauaji ya lboni, mwanaume anayekadiriwa kuwa na miaka 25 hadi 35, yaliyofanyika katika Kijiji cha Nabala, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kati ya Mei 19 na 22, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mboya, wauaji hao walikatakata viungo vya marehemu na kuuacha mwili wake ukiwa mtupu, na kwamba mabaki yake yamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kutokana na kutotambuliwa na ndugu zake.
“UTSS inalaani vikali vitendo vya ukatili na vya kinyama vya mauaji vinavyofanywa kwa walemavu hawa nchini. Katika kipindi hiki cha Machi hadi Juni mwaka huu, kumeripotiwa matukio sita ya uhalifu dhidi ya binadamu unaotishia maisha ya wenzetu wenye hali hiyo ya kurithi,” alisema Mboya.
Naye Ofisa Mshauri wa UTSS, Kondo Seif alisema suala hilo limekuwa tatizo kubwa, na kwamba inashangaza kuona serikali hailitangazi kuwa janga la kitaifa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment