Home » » Barua za Wasomaji : Wanakijiji Kimbiji tunaporwa viwanja na JWTZ.

Barua za Wasomaji : Wanakijiji Kimbiji tunaporwa viwanja na JWTZ.

Mhariri 

Sisi wanakijiji wa Kimbiji Wilayani Temeke nje kidogo ya jiji la Dar-es-salaam, tumekuwa tukipata usumbufu wa vitisho na kuharibiwa mazao na makazi yetu kutoka baadhi ya askari wa JWTZ ambao wanania ya kutaka kuyachukua maeneo ya wanakijiji chetu kwa kutumia nembo ya Jeshi (JWTZ) kinyume cha sheria.

Kuanzia mwaka jana 2011 askari wa JWTZ wamekuwa na tabia ya kuvamia mashamba ya wanakijiji  Kimbiji na kuvunja makazi ya wananchi ambao wameipigia kura serikali ya awamu ya nne huku vyombo vya dola vikiwa vimenyamaza kimya.

Wanakijiji wa Kimbiji tunalalamikia Serikali ya wilaya mkoa hadi Serikali kuu kwa unyanyaswaji, uonevu na uharibifu unaofanywa na askari hao dhidi ya wananchi wa Kimbiji na kwamba hatutaweza kuendelea kuona vyombo vya dola vikiwa vinanyamaza kimya na huku wapiga kura walioipigia kura serikali wananyanyaswa na JWTZ.

Serikali isipo ingilia kati wanakijiji watapoteza imani kwa serikali nah ii ni kwa sababu wanakijiji wa Kimbiji wengi wetu tunazifahamu haki zetu na maeneo yetu ya asili ambayo tumekua tukiishi kama wenyeji kwa miaka mingi sasa.

Pia tunafahamu fika kuwa hakuna eneo lolote linalomilikiwa na Jeshi bali wanajeshi wanataka kuchukua mashamba na makazi ya watu kwa maslahi yao binafsi!

Tunashindwa kuelewa inakuwaje jeshi linageuka chombo cha kuangamiza na kunyanyasa wananchi na kuingilia haki zao za msingi za kuishi kwa amani jambo linalokwenda kinyume na katiba ambayo inaeleza wazi kuwa kila raia anayo haki ya kulindwa yeye pamoja na mali zake.

Hata baada ya wanakijiji kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji askari hao wa JWTZ wanajaribu kutuma barua za vitisho kwa viongozi wa kijijini ili kuwatisha viongozi hao wasilipeleke jambo hili kwenye ngazi za juu.

Cha kushangaza ni kuwa baadhi ya maofisa wa Jeshi wanatumia barua zenye nembo ya jeshi kuzipeleka katika serikali ya kijiji ili kutaka kunyang'anya maeneo ya watu.

Wanakijiji wa Kimbiji hawajawahi hata siku moja kukaa kikao na serikali au wizara ya Ardhi na kujulishwa kuwa kijiji chetu kitakuwa cha kijeshi! tangu zamani makazi na mshamba ya kimbiji ni mali ya wanakijiji, hakuna eneo la wanajeshi.

Haiwezekani wanakijiji ambao ni wakazi wa asili kuhamishwa katika ardhi yao ili kupisha maofisa wa jeshi wapewe viwanja vya kujenga makazi! kufanya hivyo ni uonevu ambao haukubaliki.

Tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi kuingilia kati mgogoro huu ili kuepusha uonevu ambao unaleta sura mbaya kwa taifa, tumechoshwa na vitisho vya mtutu wa bunduki na magwanda ya kijeshi!

Pi tunaomba taasisi za haki ya binadamu kuingilia kati mateso haya.

Wanakijiji wa Kimbiji.
Temeke, Dar es Salaam.




0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa