Home » » MDTF wajipanga kumaliza kero ya maji

MDTF wajipanga kumaliza kero ya maji


na Mwandishi wetu, muh
ASASI ya wenyeji wa Muheza waishio jijini Dar es Salaam ya Muheza Development Trust Fund (MDTF), inayojishughulisha na kuhamasisha maendeleo wilayani humo, imeeleza mikakati yake ya kutaka kutatua kero ya maji.
Mikakati hiyo iliwekwa wazi juzi na wajumbe wanne wa asasi hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao, Nicolaus Mgaya, wakati walipomtembelea Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, na kuzungumza naye juu ya uwezekano wa kutatua tatizo la maji wilayani hapa.
Viongozi hao, Twaha Msenga, Clament Mang’enya, Mariam Chambika, Gregory Mgaya, Yusuph Msumari na Ally Mkufya, walielezwa kuwa kero ya maji wialayani hapo ni kubwa.
Mkuu wa wilaya aliwaambia wajumbe hao kuwa halmashauri imetenga sh milioni 200 kwa ajili ya mradi wa visima viwili ambavyo kimoja kiko eneo la polisi na kingine kiko katika eneo la Kitisa lakini fedha hizo hazitoshi.
Alisema kuwa visima hivyo viwili vinatoa maji ya kutosha lakini zinatakiwa fedha za kujenga nyumba ya kuweka pampu, kupeleka umeme, kujenga matanki na kusambaza mabomba ili maji yawafikie wakazi wa Muheza mjini na vijijini.
Mgalu alisema kuwa kwa sasa wameandika mchanganuo wa kuomba fedha wizarani ili kutatua tatizo hilo wilayani humo ambalo limedumu kwa miaka mingi.
Naye Katibu Mkuu wa MDTF, Msenga alisema kuwa matatizo yote hayo wameyasikia na kwamba watashirikiana na halmashauri kuhakikisha tatizo hilo la maji linamalizika mara moja.
Alisema kuwa MDTF itaendelea kusaidia elimu na tatizo la maji katika wilaya hiyo kama ambavyo imekuwa ikifanya mambo mengi ikiwamo kujenga shule tatu za sekondari.
Msenga alisema kuwa tayari wameshaandika mchanganuo wa kuomba ufadhili kwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Adadi Rajabu, kampuni ya bia Tanzania (TBL) na katika balozi nyingine mbili ili kuwasaidia kuondoa tatizo la maji Muheza.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa