Na Harrieth Mandari, Dar es Salaam
CHAMA cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), kimetangaza kuanza mgomo Jumatatu ya wiki ijayo, hadi Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) itakapobadilisha mfumo wa ukamataji madereva wanaokiuka sheria za barabarani.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa DARCOBOA, Sabri Mabrouk, alisema wamiliki wa mabasi madogo ya kusafirishia abiria (daladala) wamechoshwa na matatizo na malalamiko wanayoyapata kutoka kwa waajiriwa wao ambapo magari hukamatwa bila mpangilio.
“Kwa kifupi sisi hatukatai kutii sheria na tunasisitiza kuwa iwapo dereva au kondakta atakamatwa akivunja sheria achukuliwe hatua, lakini siyo kupitia askari ‘maruhani’ ambao huwakamata na kuwabambikiza makosa madereva wanayodai ya zamani,” alisema Mabrouk.
Alisema askari hao wanajulikana kama ‘maruhani’, jina ambalo limetokana na kitendo cha kuendesha mpango wa kuwakamata kwa kujificha vituoni na kuwakamata madereva na kuwabambikizia makosa mengi bila mpangilio.
“Hatukatai kuwa makosa yapo, lakini kwa nini hao ‘maruhani’ wasitambulike rasmi na kukamata pale pale dereva anapokosa, badala ya kukamata kwa makosa wanayodai wamewakuta nayo ambayo mengi kwa mujibu wa madereva wetu ni ya uongo,” alisema Mabrouk.
Alisema askari hao ambao wengi wao walikuwa madereva zamani, wamekuwa wakiomba rushwa kwa lazima mara wanapowakamata na inapotokea wananyimwa wanawabambika makosa ya ziada.
Alisema ni vyema SUMATRA itamke rasmi kuwa imewaajiri na wadau wa usafiri jijini wawatambue ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima.
“Tunaishauri SUMATRA isimamie mpango huo wao wenyewe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kudhibiti uombaji rushwa kupita kiasi na kukamata magari bila mpangilio, ambapo hadi sasa zaidi ya magari 100 yameshakamatwa,” alisema Mabrouk.
Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva na Makondakta jijini Dar es Salaam (UWAMADA), Shukuru Mlawa, alisema usumbufu wanaoupata kutoka kwa askari wa ulinzi shirikishi wanaotumiwa na SUMATRA ni batili, kwa kuwa wao kama wadau hawawatambui.
Aliishauri SUMATRA kutumia kitengo cha ukaguzi badala ya askari hao ambao wamekuwa wakiendesha mpango huo bila mpangilio.
SUMATRA hivi karibuni walianza mpango wa kukamata madereva na makondakta wa daladala wanaokiuka sheria za barabarani.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment