Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WACHUNGAJI watano ambao pia ni Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuendesha na Kusimamia upatu (DECI) waliokuwa wakifanya hivyo bila kibali wamekutwa na kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Stewart Sanga wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Washitakiwa hao ni Dominick Kagendi, Jackson Mtares, Timotheo Ole Loitinye, Arbogast Kipilimba na Samuel Mtares.
Hakimu huyo alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 16 na vielelezo kadhaa kutoka upande wa mshitaka, bila kuacha shaka mahakama imewaona watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu.
Washitakiwa waliomba mahakama kuwapa nafasi ya kuwasiliana na mawakili wao ili waweze kupanga kama watatoa ushahidi kwa njia ya kiapo au la.
Katika kesi hiyo washitakiwa wanadaiwa kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume cha sheria pamoja na kupokea amana za umma bila leseni.
Washitakiwa walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment