Home » » Kizimbani kwa kutaka kuua kwa sindano ya sumu

Kizimbani kwa kutaka kuua kwa sindano ya sumu



Na Asifiwe George, Dar es Salaam
WATU wawili, Hussein Saidi (21), mkazi wa Tanga na Deogratus Rutaganda (52), mkazi wa Tabata Kimanga, wamefikishwa Mahakama ya Ilala kwa kosa la kujaribu kuua kwa kutumia sindano yenye dawa iitwayo Diazinon.

Wakisomewa shitaka lao na Mwendesha Mashitaka, Munde Kalombola mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda, alidai Julai 11, mwaka huu, saa tatu usiku, washitakiwa walitenda kosa la kujaribu kumuua Consolata Rutagandama kwa kutumia sindano yenye sumu.

Alisema washitakiwa kwa kutumia sindano yenye dawa hiyo walimvizia Rutagandama na kutaka kumchoma kwa lengo la kutaka kumuua.

Kwa upande wa Jamhuri ulisema upelelezi bado haujakamilika na uliomba Mahakama kupanga tarehe ya kusoma kesi hiyo ili kutoa nafasi upande wa upelelezi kufanya kazi yao.

Hata hivyo, washitakiwa walikana kosa hilo na wamerudishwa rumande kutokana na kesi yao kutotimiza masharti ya dhamana hadi Julai 30, mwaka huu itakapotajwa tena.

Aidha, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na dhamana ya Sh milioni moja kila mmoja pamoja na vitambulisho.

Wakati huohuo, mkazi wa Jangwani jijini Dar es Salaam, Austino Gasto (20), amefikishwa Mahakama ya Ilala kwa kosa la kujaribu kubaka.

Akisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka, Credo Rugajo, mbele ya Hakimu Pamela Kalala, alidai Julai 6, mwaka huu, mtuhumiwa alitaka kumbaka Anita Jafesi (18) huko katika maeneo ya Ocean Road, karibu na Hospitali ya Aga Khan.

Kwa upande wa Jamhuri, ulidai upelelezi bado haujakamilika na uliomba Mahakama kupanga tarehe ya kusoma kesi hiyo ili kutoa nafasi kwa upande wa upelelezi kufanya kazi yake.

Mshitakiwa alikana kosa hilo na amerudishwa rumande kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana hadi Julai 25, mwaka huu, itakapotajwa tena.

Washitakiwa walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na dhamana ya Sh milioni moja kila mmoja pamoja na vitambulisho.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa