Home » » Kikongwe ‘ampiga singi’ shahidi mahakamani

Kikongwe ‘ampiga singi’ shahidi mahakamani


Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
KIKONGWE amenusurika kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na umri wake, baada ya kumpiga singi shahidi aliyekuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kusafirisha binadamu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Salex Tannery Ltd, Salim Ally (60).

Ushahidi ulianza kutolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mashahidi wawili upande wa mashitaka walifanikiwa kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi, Illivin Mugeta.

Wakati shahidi wa pili, Raufu Byabato, akiendelea kutoa ushahidi akieleza jinsi walivyonyanyasika nchini Yemen hadi kufikia hatua ya kuwa ombaomba, aliingia mzee huyo wa Kiarabu asiyeweza kutembea vizuri kutokana na umri wake.

Kikongwe huyo ambaye ni ndugu wa mshitakiwa, aliingia na kupishwa mahali pa kukaa na wasikilizaji wengine, alikaa katika benchi nyuma ya shahidi kwa muda wa nusu saa akisikiliza kesi hiyo, ndipo alipoinua mkono wake na kumsukumiza singi kichwani shahidi.

Shahidi aliyekuwa akitoa ushahidi huku analia aliendelea kutokwa na machozi, huku ndugu wa mshitakiwa wakisaidiana kumshika mkono mzee huyo na kumtoa nje.

“Huyu mzee asirudi tena mahakamani,” hayo yalikuwa maneno ya askari magereza aliyesimama mlangoni kwa ajili ya usalama.

“Shahidi huyu ni mzee tumsamehe, punguza hasira. Ninahitaji ulinzi kwa shahidi wangu, rudi nyuma,” hakimu alitoa amri hiyo kwa mzee mwingine aliyetaka kukaa nafasi iliyoachwa na kikongwe aliyetolewa nje.

Byabato aliendelea kutoa ushahidi ambapo alidai walikwenda Yemen kwa makubaliano ya kujenga nyumba ya mshitakiwa Januari, 2010 na walikaa huko kwa miezi sita bila malipo yoyote, japo kazi walifanya katika nyumba za mshitakiwa.

“Tulikaa miezi sita Yemen, tulijenga ghorofa moja yenye vyumba 56 na nguzo 80, tulifanya ukarabati wa nyumba ya Mzee Salim, lakini hatukulipwa ujira wowote na tulipomwambia Abdulswamad kwamba hatufanyi kazi tena akatuambia tuendelee hatutadhulumiwa malipo yetu,” alidai Byabato.

Alidai Abdulswamad waliyekwenda naye ndiye aliyepaswa kuwalipa fedha hizo, kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa kakubaliana na mshtakiwa kwamba kuna kazi Yemen na kwamba hajui walikubaliana malipo kiasi gani.

Shahidi alidai chumba walichokuwa wamefikia na huduma ya chakula waliyokuwa wakipata bila kujua aliyekuwa akilipa gharama hizo, vyote baada ya muda vilisitishwa, hivyo walikuwa wanaomba omba misaada kwa watu mbalimbali wakiwamo marafiki wa mshitakiwa na viongozi wa msikitini.

“Tuliishi kwa kusaidiwa, hati zetu za kusafiria zilichukuliwa, tulianza kuuza vifaa vya kazi ikiwamo jenereta, mashine ya kukatia vigae na mashine ya kukata vyuma,” alidai shahidi huku anabubujikwa na machozi.

Alidai baada ya kushindikana kupata malipo yao kutoka kwa mshitakiwa walikwenda kutoa taarifa polisi na kwa mkuu wa mkoa ambapo walipewa barua ya kuwasaidia kupata haki yao lakini hawakufanikiwa.

Byabato alidai alitafuta namba ya simu ya mjomba wake, Kanali Ngimela Lubinga akampigia kwa ajili ya kuomba msaada wa kurudi walikotoka.

Kanali Lubinga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, alisaidia kutoa taarifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya kuwasaidia waweze kurudi nchini.

DC Lumbinga alifanikiwa kuwapatia msaada walalamikaji wakapata hati zao za kusafiria na walirudishwa kwa msaada hadi Dar es Salaam. Kesi inaendelea leo kwa mashahidi wengine kutoa ushahidi.

Upande wa mashitaka katika kesi hiyo unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila na upande wa utetezi unaongozwa na wakili Majura Magafu.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa Agosti 8, 2010, mshitakiwa alimsafirisha Abduswamadu Omary kutoka Tanzania kwenda Yemen kwa kusingizia kuwa anakwenda kumtafutia ajira na badala yake alimtumikisha kazi za lazima.

Ilidaiwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 4 kidogo cha (1) (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2008 cha kuzuia kusafirisha binadamu.
Chanzo: Mtanzania


0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa