Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Madereva walalamikia uhamasishaji wa Sensa

Madereva walalamikia uhamasishaji wa Sensa



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BAADHI ya madereva wa malori wanaofanya safari zao kati ya Tanzania na nchi jirani, wameshangazwa na uhamasishaji mdogo kuhusiana na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, madereva hao walisema licha ya kubaki takriban siku 40, wanashangazwa Ofisi ya Takwimu ya Taifa kulipa uzito wa chini zoezi hilo linalofanyika kila baada ya miaka kumi. 

Mmoja wa madereva hao, Abdulaziz Tariq, alisema Sensa ni nguzo kuu ya mipango ya nchi na wananchi wake kwa miaka 10 ijayo, lakini haipewi kipaumbele na badala yake inatangazwa kama disco la sikukuu au tangazo la kukaribisha mwenge. 

“Zamani sensa inapowadia vyombo vyote vya habari kwa mkakati mmoja, vilikuwa vikitangaza na kuhamasisha watu kuwepo kwenye makazi yao.

“Pia kuelewesha wale wenye maswali kuhusiana na zoezi zima, inasikitisha mwaka huu zoezi hili linapochukuliwa kama ni shughuli ya mtaa au kata,” alisema Tariq. 

Naye Sadick Mohamed, dereva wa Kampuni ya Swanlinks International, amehoji yalikokwenda matangazo ya zabuni kutafuta kampuni zenye uwezo na utaalamu wa kuandaa zoezi la uhamasishaji la kitaifa kuanzia ngazi ya mikoa hadi kata. 

“Mara nyingi sisi tumekuwa tunasafiri, hivyo tunahitaji taarifa sahihi kuhusiana na zoezi hili. Hata hivyo siku zimepita kuelekea kwenye sensa bado naona kimya. Je wafadhili waliokuwa wanafadhili mpango huo wamejitoa?, Au labda haikutokea kampuni yenye uwezo wa kufanya kampeni hiyo?,” alihoji Mohamed. 

Kufuatia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori nchini CHAMAMATA, Clement Masanja aliomba suala hilo lipatiwe ufumbuzi muda mfupi uliobaki kabla zoezi hili halijafanyika.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa