Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imelalamikiwa kushindwa kuondoa mabango ya waganga wa tiba za asili na hali hiyo inazidisha kushusha heshima ya tiba za asili nchini.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Utabibu na Dawa za Asili Tanzania (ATME), Simba Abraham.
Alisema Serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilitoa amri ya kuondolewa kwa mabango yote ya waganga wa tiba za asili yaliyokuwa na ujumbe unaopotosha jamii, ikiwamo kushawishi mauaji ya albino.
“Toka Pinda atoe maagizo haya hatuoni mabadiliko, sana sana tunaona mabango ya kupotosha jamii ya waganga wa jadi ndiyo yanaongezeka, suala hili tumelipigia kelele kwa wenzetu wa Baraza la Tiba Asili Tanzania, lakini hadi leo hatuoni hatua zozote zinachukuliwa.
“Aprili 7, mwaka huu, tulikuwa na kikao na watu wa Baraza la Tiba Asili ambalo liko chini ya Wizara ya Afya, tuliwaeleza malalamiko yetu, walisema hatua za kuondoa mabango hayo zitafanyika haraka iwezekanavyo, lakini hadi leo hii mabango bado yapo na kibaya zaidi viongozi wa ATME tunatumiwa ujumbe wa vitisho kwamba sisi ndiyo tunang’ang’ania mabango yatoke na ipo siku tutakiona cha moto,” alisema Simba.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment