Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SEKTA BINAFSI ZATAKIWA KUACHA KUTOA RUSHWA

SEKTA BINAFSI ZATAKIWA KUACHA KUTOA RUSHWA



Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
SEKTA binafsi nchini zimetakiwa kuacha kutoa rushwa kwa watumishi wa Serikali na sekta nyingine binafsi kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya rushwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika Mkutano wa 13 wa kujadili Katiba ya sekta binafsi, Mwenyekiti wa African Life, Balozi Ibrahim Kaduma, alisema watoaji wa rushwa wengi wako sekta binafsi, hivyo imefika wakati wa kusema basi na hatimaye wakate mizizi.

Alisema suala la rushwa katika sekta binafsi linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushawishi wa kupata huduma katika ofisi mbalimbali pamoja na zabuni.

“Sekta binafsi mna nafasi za kuzuia rushwa na ifike wakati mseme sasa basi, kataeni kutoa rushwa kwa maofisa mbalimbali wanaowaomba, hii itasaidia kukomesha vitendo hivi,” alisema Kaduma.

Alisema wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, vitendo vya rushwa havikuwapo na hiyo ilitokana na kufundishwa ahadi za TANU na kuzizingatia.

Alisema ni wakati muafaka kwa wafadhili kutoa masharti nafuu yatakayoweza kuziinua sekta binafsi pamoja na kunyanyua uchumi wa nchi.

Aliwataka wadau wa sekta binafsi kuweka malengo ya kuunda mfuko maalumu utakaosaidia kunyanyua maendeleo ya nchi, ikiwamo kuwekeza katika masuala ya elimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Sembeye, aliiomba Serikali kuwatengenezea mazingira mazuri kuondokana na adha wazipatazo hivi sasa.

Alisema mazingira ya uwekezaji yanatakiwa kuangaliwa upya na kuboreshwa, ikiwa ni pamoja na kutupia macho kwa wafanyakazi wa migodini ambao wamekuwa wakiteseka siku hadi siku kutokana na mikataba mibovu.

Alisema Serikali inatakiwa ifanye jitihada za kusimamia wafanyakazi wa migodini na waweze kuwa na pensheni na hatimaye ziwasaidie pindi wanapopata matatizo mbalimbali wawapo kazini.

“Mazingira ya sekta binafsi si mazuri na yanahitaji maboresho, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa, hivyo imefika wakati sheria zikaangaliwa upya,” alisema.

Hata hivyo wanachama wa sekta binafsi kwa pamoja wameazimia kuunda chama chao kitakachokuwa kinasimamiwa na serikali.

Chanzo: Mtanzania


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa