Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imetoa tahadhari ya ugonjwa wa Ebola kwa wananchi wote, hususan wale waliopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ya Uganda.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu, Regina Kikuli, inasema wamepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.
Taarifa hiyo, ilisema maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo, ni kanda ya Magharibi na kwamba tayari watu 20 wamepata maambukizi na kati yao, 14 wamepoteza maisha.
Alisema mikoa ambayo inapaswa kuchukua tahadhari hiyo ni Mara, Mwanza, Kigoma na Rukwa.
Alisema chanzo cha ugonjwa huo, ni virusi vya Ebola na dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kutoka vidonda kooni.
“Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele kwenye ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje ya mwili.”
Alisema kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku mbili hadi 21, baada ya kupata maambukizi.
Taarifa hiyo, ilisema ugonjwa huo unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa njia mbalimbali, ikiwemo kugusa damu na majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa.
Aina nyingine ni kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu na kugusa wanyama walioambukizwa kama vile sokwe na swala mwitu.
Alisema ugonjwa huu hadi sasa, hauna tiba wala chanjo na kwamba wizara imechukua tahadhari mbalimbali, ikiwemo kutoa taarifa za kuenea kwa ugonjwa.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment